Magaidi wawili kukaa jela miaka 19 kwa kupatikana na silaha hatari
NA RICHARD MUNGUTI
MAGAIDI wawili wamehukumiwa kifungo cha kukaa jela miaka 25 kwa kupatikana na silaha hatari walizonuia kutumia kulipua Mahakama ya Milimani, jumba la mikutano ya kimataifa la KICC na asasi nyingine za serikali.
Lakini hakimu mwandamizi Zainab Abdul alipunguza kifungo kwa miaka sita waliyokaa gerezani kesi ikiendelea.
Sasa watatumika kifungo cha miaka 19 kila mmoja.
Abdulmajit Hassan Adan na Mohamed Osman Nane, walisukumiwa kifungo hicho na Bi Abdul baada ya kuwapata na hatia ya kumiliki gruneti 36, bunduki tano aina ya AK-47 na gari lililokuwa na vilipuzi.
Na wakati huo huo, hakimu alimsukumia kifungo cha miaka mitatu jela afisa wa kupeana vitambulisho vya kitaifa Bi Lydia Nyawira Mburu kwa kuwahudumia magaidi hao.
Hakimu alisema kitambulisho kimoja kilipatikana na gaidi aliyeuawa Osman Abdi Huga.
Hakimu aliwapongeza maafisa wa polisi waliowatia nguvuni Adan na Nane katika eneo la Merti, Kaunti ya Isiolo mnamo Februari 15, 2018, wakiajiandaa kutekeleza uhalifu.
Hakimu alisema silaha hizo zingesababisha maafa makubwa endapo hazingetunguliwa.
Akijitetea Adan alisema: “Namshukuru Mungu kwa vile silaha hizi hatari hazikuwa zimelipuliwa na watu wasio na hatia kuaga dunia.”
Aliomba mahakama imkabidhi kifungo cha nje ndipo “nipate fursa ya kuhubiri kuhusu athari za ugaidi nchini Kenya, Afghanistan, na Syria.”
“Naomba hii mahakama inipe muda niwahubirie watu athari za ugaidi na maisha ya uhalifu. Kamwe uhalifu haulipi,” akamrai hakimu.
Hakimu aliombwa na kiongozi wa mashtaka Allan Mulama awasukumie magaidi hao kifungo cha maisha gerezani kwa vile wangesababisha maafa makubwa.