Habari za Kitaifa

Magavana 4 taabani kuhusiana na ufisadi

Na Na NDUBI MOTURI August 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) inapendekeza magavana wanne wa kaunti washtakiwe kwa kukiuka maadili ya ofisi zao.Mkurugenzi Mkuu wa EACC, Abdi Mohamud, alisema kuwa tume hiyo kwa sasa inachunguza magavana wengine watano walio mamlakani na 11 wa zamani kuhusiana na madai ya mgongano wa maslahi na ulanguzi wa fedha.

Aidha, tume hiyo inashughulikia kesi za thamani ya Sh1.6 bilioni zinazohusisha maafisa wa kaunti 822.“Uchunguzi huu unahusu madai ya ubadhirifu wa fedha za umma, mgongano wa maslahi, ulanguzi wa fedha, na umiliki wa mali ambayo haieleweki walivyoipata, miongoni mwa makosa mengine chini ya Sheria ya Kupambana na Ufisadi na Uhalifu wa Kiuchumi,” alisema Bw Mohamud.

Miongoni mwa magavana ambao faili zao za uchunguzi tayari zimekamilika na kuwasilishwa kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) ni Kimani Wamatangi (Kaunti ya Kiambu), Prof Hillary Barchok (Bomet), na Mohamud Ali (Marsabit).

Katika Kaunti ya Kiambu, EACC inadai kuwa Bw Wamatangi alihusika katika kashfa ya kandarasi ya thamani ya Sh1.27 bilioni ambapo kampuni zinazohusishwa na mkewe, watoto wake, na dada yake zilipokea zabuni akiwa Seneta.

Ripoti ya EACC iliyowasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma inamlaumu gavana huyo kwa mgongano wa maslahi, ununuzi haramu wa mali ya umma, na kulangua fedha zilizopatikana kwa njia ya uhalifu.

Kashfa hiyo inadaiwa kufanyika kati ya 2017 na 2022, wakati Wamatangi alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Barabara na Usafiri ya Seneti, nafasi iliyompa mamlaka ya moja kwa moja ya kusimamia KeNHA na KURA.

Badala ya kuyawajibisha mashirika hayo mawili, EACC inadai kuwa alitumia nafasi hiyo kufanikisha zabuni kwa kampuni ambapo watu wa familia yake waliorodheshwa kama wakurugenzi, lakini akaunti za benki zilikuwa chini ya usimamizi wake binafsi.Katika ripoti yake, EACC ilipendekeza mashtaka dhidi ya Gavana Wamatangi, mkewe, dada yake na washirika wao waliotajwa kama washukiwa wenza.

EACC imependekeza mashtaka dhidi ya Gavana wa Bomet, Prof Hillary Barchok, kwa madai ya kuhusika katika sakata ya Sh152 milioni iliyohusisha kampuni za jamaa na marafiki wa karibu.

Kulingana na uchunguzi wa EACC, kampuni sita zilizopewa zabuni na Kaunti ya Bomet kati ya mwaka wa 2019 na 2025 zilihusishwa moja kwa moja na akaunti binafsi za familia ya gavana.

EACC pia inapendekeza mashtaka dhidi ya Gavana wa zamani wa Bungoma, Wycliffe Wangamati, kwa madai ya zabuni kwa kampuni hewa zilizohusiana na ndugu zake.

Wangamati, pamoja na Mbunge wa Webuye Magharibi na maafisa wa kaunti na wakandarasi kadhaa, wanakabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya mamlaka, mgongano wa maslahi, kupata zabuni kinyume cha sheria.

Katika Kaunti ya Marsabit, EACC inasema kuwa kati ya 2017 na 2024, kampuni sita zinazohusiana na Gavana Mohamud Ali, wake zake wawili, Seneta Mohamed Said Chute, na washirika wao walipokea zabuni 104 za thamani ya karibu Sh728 milioni.