Habari za Kitaifa

Magavana Pwani sasa wabanwa kuhusu mabilioni umaskini ukitesa wakazi

Na WINNIE ATIENO January 26th, 2026 Kusoma ni dakika: 3

MAGAVANA wanne kutoka eneo la Pwani walijikuta pabaya baada ya maseneta kuanza kuchunguza madai kuhusu uozo wa kifedha, ufisadi na ukiukaji wa sheria hasa katika sekta za maji na afya.

Walipofika mbele ya Kamati ya Seneti inayosimamia Uwekezaji wa Kaunti, Magavana Abdulswamad Nassir (Mombasa), Gideon Mung’aro (Kilifi), Issa Timamy (Lamu) na Dhado Godhana (Tana River) walitatizika kueleza namna mabilioni ya fedha za umma yamepotea au kutumiwa vibaya katika sekta hizo muhimu.

Katika vikao tofauti vilivyofanyika Nairobi wiki iliyopita, magavana hao walitakiwa kuelezea jinsi mabilioni ya fedha za umma yalitumika ilhali hakuna stakabadhi za kuthibitisha matumizi, au zimetumiwa vibaya katika hospitali na mashirika ya maji.

Gavana Nassir alikumbana na ghadhabu ya kamati hiyo baada ya kubainika kuwa, Hospitali Kuu ya Mafunzo na Rufaa ya Pwani (CGTRH), almaarufu kama Makadara, imekuwa ikikaidi sheria kwa kutowasilisha ripoti za kifedha kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (OAG) kila mwaka.

“Hii si mara ya kwanza. Imekuwa kama hulka sasa kutoka kwa hospitali hiyo. Kila mwaka, hospitali hii imekuwa ikipuuza afisi ya mkaguzi wa fedha za umma.

“Wakazi wa Mombasa wana haki ya kujua namna fedha zao zinatumika,” alisema Seneta wa Vihiga, Bw Godfrey Osotsi, ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati hiyo.

Seneta wa Migori, Bw Eddy Oketch, aliitaka serikali hiyo iwachukuliwe hatua kali za kisheria maafisa wa hospitali hiyo ambayo ndiyo kubwa zaidi katika eneo la Pwani.

Hata hivyo, Gavana Nassir alieleza kuwa, aliwasimamisha kazi maafisa wawili.

Hali ilikuwa mbaya zaidi katika kampuni ya kusambaza maji ya Mombasa (MOWASCO), ambayo ilipatikana imefilisika ikiwa na deni la Sh2.26 bilioni.

Kamati hiyo ilishtuka baada ya kuarifiwa kwamba majitaka pia huwa yanamwagwa baharini kwa kuwa mitambo ya kusafisha majitaka kabla yaachiliwe baharini haifanyi kazi.

Seneta Peris Tobiko alimshtumu Gavana Nassir kwa kukosa kuwajibikia hali hiyo, akisema ni uchafuzi wa mazingira na ukiukaji wa haki za binadamu.

“Je, mnajua kuwa mnahatarisha maisha ya umma? Watu wanaogelea kwenye maji yaliyochafuliwa na kinyesi cha binadamu, na wavuvi wanavua samaki?” aliuliza Bi Tobiko.

Hata hivyo, Bw Nassir alijitetea akisema kuna miradi inayoendelea ya ukarabati inayofadhiliwa na Benki ya Dunia inayotarajiwa kukamilika Oktoba 2026.

Maseneta walitaka hatua za haraka zichukuliwe, wakisema haifai wananchi kuendelea kukaa katika mazingira machafu kwa miezi tisa zaidi wakisubiri hatua zichukuliwe.

“Tutaendelea kushirikiana na seneti na taasisi zote za kutathmini matumizi ya fedha za umma ili kuimarisha utendakazi na matumizi bora ya fedha za umma,” alisema Bw Nassir kwenye taarifa baadaye.

Wakati wa zamu ya Gavana Mung’aro ulipofika, kamati hiyo ilitaka kujua kuhusu ongezeko la kutatanisha la maji yanayotumiwa bila kulipiwa.

Katika kampuni ya Malindi Water, kamati hiyo inachunguza ripoti ya mkaguzi wa hesabu kuwa, katika kipindi cha mwaka mmoja tu asilimia ya maji yaliyotumiwa bila kulipiwa ilikuwa 42 kutoka asilimia 16 mwaka uliotangulia.

“Ongezeko hili si la kawaida, huu ni wizi wa maksudi,” alisema Seneta Osotsi.

Licha ya Bw Mung’aro kuomba muda wa kurekebisha hali hiyo, kamati ilikataa maelezo yake ikisema kampuni hizo zilizofilisika zimebaki kuwa mashimo ya kupotezea pesa.

Gavana Timamy naye alitakiwa kuelezea kwa nini hoja za ukaguzi zimekuwa zikijirudia katika hospitali za Faza, Mpeketoni na ile ya rufaa ya Lamu.

Kamati hiyo ilishangazwa na ukosefu wa stakabadhi za matumizi ya fedha na usimamizi mbovu wa mali za kaunti.

Seneta wa Machakos, Bi Agnes Kavindu, alieleza masikitiko kwamba tangu mwaka wa 2023, miradi mingi ya maendeleo katika kaunti hiyo imekwama huku rekodi za uhasibu zikiwa na makosa ya kimsingi.

Kwa upande wake, Gavana Godhana alijitetea kuhusu masuala yaliyoibuka katika ripoti ya mkaguzi akisema atashirikiana na taasisi za ukaguzi ili kufanikisha ugatuzi.

Gavana wa Kwale, Bi Achani, alihojiwa kuhusu usimamizi wa manispaa za kaunti hiyo.

Hata hivyo, Bi Achani alilalamika kuhusu uhaba wa wafanyikazi hasa katika hospitali za kaunti na shule za chekechea.