Habari za Kitaifa

Magavana wa zamani kusomewa ‘dhambi’ zao mbele ya Seneti

May 23rd, 2024 2 min read

NA MARY WANGARI

MAGAVANA wa zamani huenda sasa wakalazimika kuanza kufika mbele ya Seneti kujibu maswali yanayoibuka katika ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Nancy Gathungu kuhusu hatamu walizohudumu kama wakuu wa kaunti.

Kwa muda sasa, Bunge la Seneti limekuwa likijipata kwenye njia panda huku magavana wapya kadhaa wakishindwa kujibu masuala yaliyojiri kabla ya wao kuchukua usukani.

Kisii ni mojawapo ya zilizoathirika huku Gavana Simba Arati akishindwa kujibu maswali kuhusu matumizi ya fedha ambazo kaunti hiyo ilipokea katika bajeti za kuanzia 2019 hadi 2022.

Ripoti ya mkaguzi imemulika serikali ya Kaunti ya Kisii kuhusiana na Sh416.5 milioni za basari zilizotengewa kaunti hiyo katika utawala wa aliyekuwa gavana James Ongwae.

“Ni Sh7.2 milioni pekee zilizosambaziwa wanafunzi huku fedha zilizosalia zikitumika kwa shughuli nyingine ambazo hazikustahili,” alisema mkaguzi.

Isitoshe, serikali ya Kaunti ya Kisii ilishindwa kufafanua sababu ya kukosa kutoa basari licha ya kupokea Sh135 milioni zilizotengewa basari katika mgao wa bajeti kwenye mwaka wa kifedha uliokamilika Juni 30, 2020.

Kaunti hiyo ilipokea Sh3,286,789 za basari kufadhili elimu ya wanafunzi maskini wa sekondari lakini hakukuwa na risiti za kuthibitisha jumla ya Sh2,742,789 zilizotolewa kama basari katika taasisi mbalimbali.

Katika bajeti iliyokamilika Juni 2022, hazina ya basari ilitumia Sh520,000 hata baada ya kupokea kitita cha Sh11 milioni zilizoidhinishwa kusambazwa kama basari huku Sh10,480,000 (asilimia 95) zikikosa kutumika.

“Taarifa ziliashiria tofauti kati ya bajeti asilia na kiasi kilichotumika. Hazina ya Basari ilisambaza Sh. 3,419,047 kinyume na bajeti iliyoidhinishwa ya Sh 135,000,000 hivyo kiasi kilichotumika kwa basari kilipunguzwa kwa asilmia 98 sawa na Sh.131,580,953,” ilisema ripoti.

Hali hiyo huenda ilisababisha wanafunzi maskini Kisii kukosa ufadhili wa kuendelea kielimu na kuathiri matokeo yao kwenye mitihani, alihoji Mkaguzi Mkuu.

Akizungumza katika kikao cha Seneti ambapo Gavana Arati alialikwa kujibu maswali, Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Matumizi ya Fedha za Umma, Godfrey Osotsi (seneta wa Vihiga) alisema pana haja kubwa ya kuwaagiza maafisa wa zamani kufika mbele ya kamati hiyo.

Seneta huyo wa Kaunti ya Vihiga alisema japo serikali zote za kaunti 47 huendesha shughuli zake bila kukatizwa, wakati umewadia kwa maafisa kuwajibikia binafsi masuala yanayohusu kipindi walichohudumu.

“Huenda sasa kama Kamati tukamwalika aliyekuwa Gavana wa Kisii, kufafanua jinsi mamilioni yaliyotengewa hazina mbalimbali za kaunti zilivyotumika kati ya 2019 na 2022 alipokuwa akihudumu. Gavana mpya wa sasa ameshindwa kueleza nini hasa kilitendeka,” alisema Seneta Osotsi.

Kwa upande wake, Gavana Arati alieleza Kamati kwamba ametenga kiasi cha Sh245 milioni za basari katika bajeti ya mwaka huu 2024 ambapo wadi zote 45 zimepokea Sh45 milioni kila mmoja, ikiwemo mikakati ya kuhakikisha wanaostahili pekee wanaopata ufadhili huo.