Habari za Kitaifa

Magavana walalama serikali inawahujumu

February 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WINNIE ATIENO

MAGAVANA wamekasirishwa na kile wanachokitaja kama mwenendo wa serikali ya kitaifa kuhujumu uwezo wao wa kutekeleza majukumu yao ya kikatiba.

Kulingana na barua ambayo tuna nakala yake, baraza la Magavana (CoG) limeorodhesha malalamishi kadha ambayo yatajadiliwa katika mkutano wa dharura utakaofanyika Alhamisi ijayo.

Kando na kukiuka Katiba kwa kutwaa majukumu yaliyogatuliwa, CoG inayoongozwa na Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru, inakerwa na hatua ya serikali ya kitaifa kupuuza maafisa wa kaunti wakati wa utekelezaji wa majukumu yaliyogatuliwa kama vile Afya, Nyumba, Huduma za Maji na Biashara.

“Hujuma hizo zinaendelezwa kila siku, haswa kupitia kutolewa kwa mgao wa bajeti kwa majukumu yaliyogatuliwa kulipitia Wizara, Idara na mashirika ya serikali ya kitaifa,” CoG inaeleza katika barua yake.

Wakuu hao wa kaunti 47 pia wanaisuta Serikali ya Kitaifa kwa kuwatumia Wabunge, kimasukudi, katika utekelezaji wa mipango na miradi iliyogatuliwa, kinyume na hitaji la katiba.

Hali hii, wanasema, inawaacha maafisa wa serikali za kaunti wakiwa wamechanganyikiwa kuhusiana na iwapo wao ndio watawajibikia makosa ibuka au la.

Kwa mfano, Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir aliishutumu Wizara ya Maji kwa kuvuka mipaka ya majukumu yake.

Bw Nassir alitaja Mpangilio wa 4, Sehemu ya 11 (b) kwenye Katiba unaosema wazi kuwa, shughuli za utoaji huduma za maji na usafi zinapasa kuendeshwa na serikali za kaunti.

“Hatua ya Serikali ya Kitaifa kutekeleza miradi ya maji katika maeneo bunge ni kinyume cha Katiba na ni haramu,” Bw Nassir akasema Ijumaa wakati wa mkutano wa mashauriano ulioshirikisha wadai wakiwemo maseneta, magavana na maafisa wa mashirika ya maji yanayosimamiwa na Serikali ya Kitaifa.

Gavana huyo wa Mombasa alionya kuwa, suala hilo linaweza kusababisha mivutano ya kimamlaka kati ya Magavana na Wabunge.

“Ikiwa kuna rasilimali za ziada, zielekezwe kwa serikali za kaunti kama mgao wa fedha za utekelezaji wa majukumu mahsusi (Conditional Grants),” Bw Nassir akashauri.

CoG inalalamika kuwa, licha ya kwamba imetuma nyaraka nyingi kwa asasi mbali mbali za serikali ya Rais William Ruto, juhudi za kutimizwa kwa matakwa yao hazijazaa matunda.

“Kwa misingi hii, CoG imefanya mkutano na Magavana wanaowakilisha sekta zilizoathirika na tatizo hili ili kujadili njia bora za kulitatua,” CoG ikasema.

Miongoni mwa ajenda za mkutano huo ni utekelezaji wa Mpango wa Ustawishaji Masoko, Mpango wa Nyumba za Gharama Nafuu na Mswada wa Nyumba za Gharama Nafuu ya 2023 na Mpango wa Utoaji Huduma Nafuu za Afya.

Kulingana na Katiba ya sasa, majukumu haya matatu yamegatuliwa.

Magavana hao pia watajadili malipo ya marupurupu na Wizara ya Afya kwa Maafisa wa Afya ya Kijamii (CHPs), Utoaji wa Mgao wa Fedha za Bajeti kwa Kaunti kwa wakati na athari za sheria tatu za afya zilizopitishwa na Bunge la Kitaifa mwaka 2023.

Kulingana na magavana, maafisa hao wa CHPs huenda wakatumiwa vibaya na serikali ya kitaifa kuendeleza ajenda zake sawa na jinsi Rais (Mstaafu) Uhuru Kenyatta aliwatumia machifu kama vyombo vya kuendeleza ajenda zake za kisiasa.

Ijumaa wiki hii, magavana wote, akiwemo Bi Waiguru, walikaidi mwaliko wa Naibu Rais Rigathi Gachagua wa kuhudhuria mkutano wa uzinduzi wa mpango wa malipo kwa maafisa wa CHPs.

Shughuli hiyo iliandaliwa katika makazi rasmi ya Naibu Rais mtaa wa Karen, Nairobi.

Kulingana na mpango huo, maafisa hao wa afya ya kijamii watakuwa wakipokea marupurupu ya Sh5,000 kila mwezi kutoka kwa serikali ya kitaifa.

Serikali za Kaunti pia zinapaswa kuwalipa kiasi kama hicho cha fedha na hivyo kuchangia hao kupokea jumla ya Sh10,000 kila mwezi kama marupurupu.