Magavana wakaa ngumu, wanataka mgao wa Sh439bn kuwasitiri dhidi ya ushuru wa juu
MAGAVANA wamekataa mgao wa bajeti wa Sh391.1 bilioni uliopitishwa na wabunge wakishikilia kuwa hawatakubali mgao usiopungua Sh439.5 bilioni.
Wakuu hao wa serikali za kaunti wanasema kuwa wanakabiliwa na gharama nyingine za lazima ambazo zitaongeza kwa Sh20 bilioni kiasi cha pesa wanazohitaji kugharimia mahitaji ya serikali zao katika mwaka unaokamilika Juni 2025.
Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG), Anne Waiguru, Jumanne aliwaambia maseneta kwamba serikali za kaunti zinakabiliwa na mzigo mzito wa gharama ya mishahara na malimbikizi ya madeni.
“Mzigo wa mishahara unatarajiwa kuongezeka hata zaidi kufuatia kuanzishwa kwa ushuru mpya wa nyumba na kupandishwa viwango vya makato mengine,” Bi Waiguru akasema alipofika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Fedha.
Gavana huyo wa Kirinyaga aliongeza kuwa ushuru huo wa nyumba utapandisha matumizi ya serikali za kaunti kwa kiwango cha hadi Sh4 bilioni huku makato ya Hazina ya Kitaifa ya Malipo ya Uzeeni (NSSF) yakizigharimu serikali za kaunti Sh3 bilioni zaidi.
Kulingana na Sheria ya Fedha ya 2023, kila mfanyakazi anapaswa kulipa ushuru wa nyumba za kiwango cha asilimia 1.5 ya mshahara wake kila mwezi huku mwajiri akitakiwa pia kulipa kiasi sawa na hicho.
Aidha, mabadiliko ya Sheria ya NSSF yaliyoanza kutekelezwa mwaka jana yanahitaji kwamba kila mfanyakazi atachangia Sh2,000 kila mwezi kwa hazina hii kutoka kiwango cha zamani cha Sh200 kila mwezi. Waajiri nao wanapaswa kuwasilisha mchango sawa na hicho kwa kila mfanyakazi.
Isitoshe, makato kila mwezi kwa Hazina ya Bima ya Afya ya Kijamii (SHIF) yatakayoanza kutekelezwa Julai mwaka huu, yatazilazimisha serikali za kaunti kuwalipia watu masikini ambao hawajabainishwa, hali itakayowaongezea gharama zaidi.
Isitoshe, magavana wanasema nyongeza ya kila mwaka ya mishahara itaongeza gharama yao ya matumizi yao sawa na gharama ya utekelezaji wa mkataba wa makubaliano na madaktari (CBA) utakaowagharimu Sh5.8 bilioni.
Magavana wanashikilia kuwa gharama hizo zote zinafaa kujumuishwa katika mgao wa bajeti kwa kaunti katika mwaka ujao wa kifedha wa 2024/2025.
“Serikali za kaunti zitakabiliwa na changamoto kubwa zaidi katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwa maseneta watapitisha Mswada wa Ugavi wa Mapato (DoRB) ya 2024 ulivyo sasa,” akasema Bi Waiguru.
“Serikali za kaunti zinafaa kupata mgao sawa wa mapato. Hatuulizi chochote ambacho hakijakubaliwa na Katiba,” akaongeza Waiguru.
Tayari Bunge la Kitaifa limeidhinisha mgao wa Sh391.1 bilioni zitakazogawanywa kwa kaunti zote 47 katika mwaka ujao wa kifedha.
Lakini magavana wanasema kuwa mapato kutokana na ushuru yanatarajiwa kuongezeka kwa kiwango cha asilimia 15.
Hii ni sawa na ongezeko la Sh376.9 bilioni zaidi katika mapato yanayotumiwa kukadiria ugavi wa mapato kati ya serikali ya kitaifa na serikali za kaunti.
Naibu mwenyekiti wa CoG Ahmed Abdullahi, ambaye ni Gavana wa Wajir, alisema kati ya Sh376.9 bilioni, ambazo ni ongezeko ya mapato, ni Sh5.7 bilioni pekee zinaongezwa kwa Sh385.4 bilioni zilizotengewa serikali za kaunti katika mwaka huu wa kifedha.
Bw Abdullahi pia aliwakashifu wabunge kwa kukosa kuzingatia kuwa serikali za kaunti hazijakuwa zikipokea fedha kutoka Hazina ya Ukarabati wa Barabara (RMLF), mgao ambao haujashirikishwa chini ya Mswada wa Ugavi wa Mapato.