• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:55 AM
Magavana wakemewa kwa kutishia madaktari

Magavana wakemewa kwa kutishia madaktari

NA GEORGE MUNENE

MAGAVANA wameshutumiwa vikali kwa kutishia kufuta kazi madaktari wanaogoma na ambao wamelemaza huduma za afya kote nchini wakilalamikia mazingira duni ya kazi.

Katibu Mkuu wa Muungano wa Madaktari Nchini (KMPDU), Davji Atellah, ameapa kuwa madaktari hawataingiza baridi kutokana na vitisho vya wakuu wa kaunti.

Akizunguma Jumatatu, Aprili 1, 2024 katika Kaunti ya Kirinyaga, baada ya kushiriki mkutano na madaktari eneo hilo, Dkt Atellah, alikemea vikali vitisho vinavyotolewa na magavana kutoka kaunti mbalimbali ili kushinikiza madaktari kurejea kazini.

“Tunalaani vikali juhudi hizo za kuwatishia na kuwashinikiza wanachama wetu kutelekeza mapambano yetu halali kisheria ya kupigania mazingira bora ya kazi na huduma za afya kwa Wakenya wote. Madaktari wanastahili kazi yenye hadhi,” alisema Dkt Atellah.

Alisema kuwa ni jambo la kuvunja moyo kuwa badala ya kuangazia masuala muhimu yaliyotajwa na Muungano, waajiri wamegeukia mbinu za vitisho.

“Tunataka kusema wazi kuwa hakuna daktari atakayetishiwa au kushinikizwa kurejea kazini hadi masuala yote tuliyoorodhesha kwenye notisi zetu za mgomo yatakaposuluhishwa kikamilifu,” alisema.

Dkt Atellah amewataka magavana kuelekeza juhudi zao kuangazia masuala mbalimbali yanayoathiri wahudumu wa afya katika sehemu zao anuai za kazi.

“Wakati umewadia maslahi ya wahudumu wa afya na raia wanaohudumiwa kupatiwa kipaumbele. Siasa duni zinastahili kuepukwa katika utoaji huduma,” alisema.

Alionya dhidi ya kutumia vibaya maagizo ya mahakama kulazimisha Muungano kusimamisha mgomo.

 

  • Tags

You can share this post!

Wakenya wachongoana mitandaoni wakisherehekea ‘April...

Polisi mstaafu mwenye umri wa miaka 102 bado anasoma Taifa...

T L