Habari za Kitaifa

Magavana wasifu maseneta, wabunge kukubali kuwaongezea Sh9bn

May 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA CHARLES WASONGA

MWENYEKITI wa Baraza la Magavana Anne Waiguru amewapongeza maseneta na wabunge kwa kukubali kuongeza mgao wa bajeti kwa serikali za kaunti kwa Sh9 bilioni katika mwaka ujao wa kifedha.

Kwenye taarifa aliyotoa Jumanne, Gavana huyo wa Kaunti ya Kirinyaga alisema kuwa hatua hiyo sasa inaashiria kuwa serikali za kaunti zitapokea mgao wa Sh400.1 bilioni  katika mwaka wa kifedha wa 2024/2025.

Awali, Bunge la Kitaifa lilikuwa limezitengea serikali za kaunti Sh391 bilioni kama mgao wa bajeti katika mwaka huu wa kifedha walipopitisha Mswada wa Ugavi wa Fedha wa 2024 mapema Mei.

Hata hivyo, maseneta walikataa mgao huo mswada huo ulipowasilishwa katika Seneti, wakishikilia kuwa serikali za kaunti zinafaa kutengewa Sh412 bilioni.

“Baraza la Magavana lingependa kushukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Bajeti katika Seneti ikiongozwa na Seneta wa Mandera Ali Roba na wanachama wa Kamati ya Upatanishi kwa kusaidia serikali za kaunti ziweze kupata fedha nyingi katika mwaka ujao wa kifedha,” Bi Waiguru akasema kwenye taarifa hiyo kupitia akaunti yake ya mtandao wa X mnamo Jumanne.

Bi Waiguru alisema hatua hiyo ya kuziongezea serikali za kaunti mgao wa fedha zitasaidia kupiga jeki ugatuzi.

“Fedha hizo zitaelekezwa katika miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali za kaunti na yenye manufaa kwa raia,” Bi Waiguru akaeleza.

Mvutano kuhusu ugavi wa fedha kati ya serikali kuu na zile za serikali za kaunti umekuwa ukitokea kila mara wakati wa mjadala kuhusu Mswada wa Ugavi wa Fedha.

Mapema Mei, Bunge la Kitaifa lilipitisha Mswada wa Ugavi wa Fedha wa 2024 kwa kuzitengea serikali za kaunti Sh391 bilioni ilhali magavana walipendekeza mgao wa Sh450 bilioni.

Aidha, Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) ilikuwa imependekeza kuwa serikali za kaunti zitengewe Sh407 bilioni.

Kwa upande mwingine, Serikali ya Kitaifa ilitengewa Sh2.5 trilioni za mapato ya serikali katika mwaka ujao wa kifedha unaoanza Julai 1, 2024.

Wakati wa kujadiliwa kwa mswada huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Fedha Ndindi Nyoro ambaye pia ni Mbunge wa Kiharu alisema kuwa Sh391 bilioni ambazo zingetengewa serikali za kaunti zilikuwa zikiwakilisha ongezeko la Sh16.6 bilioni kutoka kwa mgao wa mwaka uliopita wa kifedha.

“Magavana hawafai kulalamika kwa sababu Sh391 bilioni ni sawa na asilimia 24.9 ya mapato ya serikali yaliyofanyiwa ukaguzi. Serikali inakabiliwa na changamoto za kifedha kutokana na ugumu wa kupata fedha katika masoko ya humu nchini na yale ya kimataifa,” akasema Bw Nyoro.

Awali, Bi  Waiguru aliyefika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Fedha, inayoongozwa na Seneta Roba, alilalamikia mwenendo wa serikali kuendelea kukwamilia fedha zinazofaa kuelekezwa kwa serikali za kaunti.

Aidha, Bi Waiguru alilalamika kuwa baadhi ya serikali za kaunti hukabiliwa na changamoto ya ulipaji wa mishahara kwa wakati  kufuatia kucheleweshwa kwa usambazaji wa fedha kutoka kwa Hazina ya Kitaifa.

“Baadhi ya kaunti nyakati nyingine hulazimika kuchukua mikopo ya riba ya juu ili kulipa wafanyakazi,” akaeleza Bi Waiguru, akielezea mantiki ya magavana kutaka mgao wa Sh450 bilioni.