Habari za Kitaifa

Magavana wataka maseneta kukataa fomula ya kugawa mapato

Na SHABAN MAKOKHA January 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MFUMO mpya wa ugavi wa mapato kwa kaunti uliopendekezwa Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA), unakabiliwa na upinzani kutoka kwa magavana huku ukisubiri kuidhinishwa na Seneti.

Baadhi ya wakuu wa kaunti wamewasiliana na Maseneta na Wabunge kuwataka wakatae fomula iliyopendekezwa kugawa Sh417 bilioni kwa kaunti Mwaka wa Kifedha wa 2025-2026.

Katika fomula iliyopendekezwa, CRA imepunguza idadi ya vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa katika kugawia kaunti pesa kutoka nane hadi tano pekee.

Fomula mpya ya CRA inasisitiza idadi ya watu huku ikiondoa vigezo vitatu muhimu vya Afya, Kilimo na Barabara katika fomula ya sasa ya ugavi wa mapato.

Zaidi ya nusu ya kaunti 47 zitapata mgao wa chini iwapo fomula iliyopendekezwa na CRA itaidhinishwa na Bunge.

Iwapo Bunge haitatenga pesa zaidi kwa kaunti zitakazoathiriwa, Kitui, Kakamega na Narok ni baadhi ya kaunti ambazo zitapunguziwa mgao.

Kwa sasa, idadi ya watu inachangia asilimia 18 pekee lakini fomula mpya imeongezeka hadi asilimia 42, usawazishaji ulipata asilimia 22 kutoka asilimia 20 na ukubwa wa kijiografia ulinufaika na ongezeko la asilimia 9.

Kaunti 31 zinatazamiwa kupunguziwa mgao huku Kakamega ikipata hasara kubwa katika fomula hiyo mpya ambayo inaweza kupelekea kaunti hiyo kupoteza Sh407 milioni.

Kwa upande mwingine, kaunti 16 zitavuna pakubwa huku kaunti ya Garissa ikinufaika zaidi na Sh1.9 bilioni zaidi katika fomula mpya.

Fomula hiyo imetumwa kwa Seneti ili kupata idhini na magavana wanasisitiza kuwa Maseneta wanapaswa kuokoa kaunti kutoka kwa shida za kifedha.

Mwenyekiti wa kamati ya Fedha katika Baraza la Magavana Fernandes Barasa anaitaka CRA kuhakikisha kuwa ugavi wa mapato hautatiza kaunti yoyote

Gavana wa Kakamega aliwataka Maseneta, kama watetezi wa ugatuzi, kukataa mfumo wowote usio na haki.

“Kama mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ya CoG, ninataka kukumbusha CRA kwamba magavana wote 47 walikubalina na kuungwa mkono na seneti kwamba hakuna kaunti yoyote inapaswa kutatizwa katika ugavi wa mapato. Tumeona kaunti za eneo la kaskazini zikiongezewa mgao ilhali zinanufaika na Hazina ya Usawazishaji. Ninatoa changamoto kwa CRA kuhakikisha kwamba hakuna kaunti yoyote itakayopoteza katika pendekezo lake kwa Seneti,” akasema Bw Barasa.

Alitoa wito kwa Maseneta kukataa fomula iliyopendekezwa akidai haina haki na usawa jinsi ilivyo katika Katiba na Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma.

Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir pia alikataa fomula iliyopendekezwa akisema kaunti za mijini zitaathiriwa vibaya na zitashindwa kutekeleza miradi.

Alisema Mombasa inatazamiwa kupoteza zaidi ya Sh250 milioni katika fomula iliyopendekezwa na hii itaathiri utoaji wa huduma katika kaunti ya Pwani.

Naye Gavana wa Samburu Lati Lelelit amepinga vikali mfumo wa ugavi wa mapato uliopendekezwa na Tume ya CRA, akiutaja kuwa hatari kwa kaunti zilizo na watu wachache kama Samburu.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA