Habari za Kitaifa

Magavana watishia kufunga kaunti zote

Na NDUBI MOTURI March 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

BARAZA la Magavana nchini (CoG) limetishia kulemaza shughuli katika kaunti 47 ikiwa serikali ya kitaifa haitabadilisha Mswada wa Ugavi wa Ziada wa Serikali za kaunti, 2025 ndani ya siku 14.

Makamu Mwenyekiti wa CoG Dkt Mutahi Kahiga Ijumaa, Machi 21, 2025 alisema serikali za kaunti zitapoteza jumla ya Sh38.4 bilioni za mgao wa ziada katika mswada huo.

Kati ya kiasi hiki Sh24 bilioni ni ruzuku ya masharti kutoka kwa wafadhili kusaidia miradi muhimu ya kaunti katika huduma za afya, kilimo, uvuvi, maji, barabara, uboreshaji wa makazi duni na ukuzaji wa miundombinu.

“Kitendo hiki cha wazi ni jaribio lingine la kulemaza utoaji wa huduma katika Serikali 47 za Kaunti, dharau kwa ajenda ya Ugatuzi kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Kenya, 2010. Hatua hii ya hivi punde si tukio la kwanza bali ni mazoea,” Dkt Kahigalls alisema.

Dkt Kahiga pia alipuuzilia mbali madai ya serikali ya kitaifa kwamba kuna upungufu wa mapato kutokana na kuondolewa kwa Mswada wa Fedha wa 2024 tangu serikali ya kitaifa ilipoongeza matumizi yake kwa Sh114 bilioni katika Sheria ya Matumizi ya Ziada, 2025.

“Hilo linatumika tu kama kisingizio ili kuuzia serikali za kaunti kupata pesa za ziada. Madai haya ya uwongo yanaonyesha jinsi Serikali ya Kitaifa inavyoshughulikia Ajenda ya Ugatuzi bila mpangilio. Ikumbukwe kwamba Kaunti tayari zimekuwa zikifadhili miradi inayoendelea,” akaongeza.

Magavana hao pia walitaka Sh78 bilioni za miezi ya Januari, Februari na Machi ziachiliwe.