Habari za Kitaifa

Mageuzi idara ya mahakama hufanywa na tume – Raila

January 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA ALEX KALAMA

KIONGOZI wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga, amekosoa hatua ya Rais William Ruto na Jaji Mkuu Martha Koome kukutana kwa mashauriano ya namna ya kumaliza jinamizi la ufisadi katika Idara ya Mahakama.

Akihutubia wajumbe wa ODM mjini Malindi katika Kaunti ya Kilifi mnamo Jumatano, Bw Odinga alisema ofisi ya Rais, inaendelea kuziteka nyara asasi muhimu za serikali, ambazo zinafaa kufanya kazi bila mwingiliano wa aina yoyote, kwa mujibu wa sheria.

Bw Odinga alidai kwamba Rais anavuruga mahakama, Bunge la Kitaifa na lile la Seneti kwa kushinikiza asasi hizo kupitisha miswada bila kuipiga msasa vilivyo.

Kuhusu mazungumzo yaliyofanyika Jumatatu baina ya ofisi ya Rais na Mahakama katika Ikulu, ambapo pia Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula alihudhuria, Bw Odinga alisema yaliendeshwa kiharamu.

Alifafanua kwamba endapo kulikuwa na kashfa yoyote katika idara ya mahakama, kulikuwa na njia nyingine za kukabili hali hiyo.

“Zipo njia muafaka za kuleta mageuzi katika Idara ya Mahakama na njia hizo ni kutumia taasisi huru au tume maalum na wala sio Rais, mahakama na bunge,” akasema Bw Odinga.

Kiongozi huyo ambaye pia ni kinara wa muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya, amedai kuwa mabunge yote mawili–la kitaifa na seneti–yameshikwa mateka na afisi ya Rais, na huendesha shughuli zao kinyume na sheria.

“Wabunge wanapitisha kila kitu ambacho kinatoka kwa Ikulu. Hakuna chochote ambacho kinabadilishwa. Miswada inapenyezwa tu bungeni na spika anaamua kwamba ni sharti ipitishwe kwa muda wa saa mbili. Hakuna kinachojadiliwa… huwezi ukajadili mswada kwa saa mbili,” akasema.

Bw Odinga hakuwasaza maspika wa mabunge hayo mawili, akisema kuwa wamekuwa wakikiuka sheria kwa kuhusishwa wakati wa Rais kutia saini miswada kuwa sheria.

“Spika hana wajibu wowote baada ya mswada kutoka bungeni. Siku hizi ninaona maspika wa Seneti na Bunge la Kitaifa wakienda kwa Ikulu na kusimama wakishuhudia Rais akitia saini miswada. Aibu kwao!” akasema.