Habari za Kitaifa

Mageuzi yalenga kuwapa baadhi ya machifu mafunzo ya kijeshi, silaha

Na  NDUBI MOTURI August 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, jana alitangaza mageuzi makubwa yanayolenga kuwapa nguvu zaidi machifu na manaibu wao, ikiwa ni pamoja na kupandishwa vyeo, mafunzo ya kuwajengea  uwezo, nyongeza ya mishahara huku baadhi yao wakitarajiwa kupewa silaha.

Machifu 8,102 kote nchini watapatiwa mafunzo ya wiki tatu kuhusu utatuzi wa mizozo kisheria na usimamizi wa usalama katika Chuo cha mafunzo ya polisi cha Embakasi. Kundi la kwanza kupatiwa mafunzo ni la machifu na manaibu machifu 1,000, na hatimaye wote waliobaki watafunzwa, baadhi yao wakihudhuria mafunzo rasmi kwa mara ya kwanza kwa zaidi ya miaka 25.

Wakati wa mafunzo hayo, baadhi ya machifu kutoka maeneo ya Kaskazini Mashariki na Bonde la Ufa watapewa mafunzo ya ziada ya kijeshi na kusajiliwa kama polisi wa akiba na pia kupewa silaha baada ya mafunzo ya hali ya juu.

“Tunaanzisha haraka mafunzo kwa wote, tukianza hapa leo,” alisema Murkomen.

Mafunzo haya pia yatawapa machifu ujuzi katika kuzuia uhalifu, kutatua migogoro ya ardhi, uhifadhi wa mazingira, na uratibu wa mashirika mbalimbali ya serikali.

“Tumeanza na mafunzo yenu, na mara tu baada ya hapo tutafuatilia kwa kuwapandisha vyeo. Masuala ya ustawi yatazingatiwa,” alisema, akiongeza kuwa machifu ni “muhimu katika utawala na muundo wa usalama wa nchi.”

Katika mkutano huo, Murkomen alilalamikia ukosefu wa mafunzo kwa machifu na manaibu wao katika tawala zilizopita, akisisitiza kuwa Rais William Ruto ameazimia kutekeleza kikamilifu mfumo wa kiuchumi wa kuanzia mashinani.

Alisema kuwa hili linaweza kufikiwa tu kwa kuwawezesha machifu na manaibu wao ambao ni kiungo kati ya ofisi ya rais na wananchi mashinani.

“Ofisi za machifu na manaibu wao mara nyingi hutambuliwa kama ofisi ya rais. Kama serikali, tumejizatiti kuboresha ofisi hizi ili wananchi wanapokuja kuhudumiwa, wajihisi wapo katika ofisi ya rais,” alisema Murkomen.

Murkomen alisema mpango huu unajibu malalamishi yaliyotolewa katika mikutano ya Jukwaa la Usalama, kama vile kutopandishwa vyeo, ugumu wa usafiri, na gharama kubwa ya kusafiri hadi Nairobi kupata sare.

Alisema kuna mipango ya kusambazwa maelfu ya sare mpya kwa kaunti, na akaahidi kupanua mpango wa kukodisha magari wa serikali ili  baadhi ya  machifu wapewe pikipiki kusaidia kazi zao.

“Nilishangaa kwamba machifu na manaibu wao wanapewa viatu vya saizi moja tu yaani saizi 5 kwa wanawake na saizi 7 kwa wanaume — na sare bila kupimwa. Tutakuwa makini zaidi; tutaanza kupima na kuhakikisha sare zinasambazwa moja kwa moja kwa kaunti badala ya nyinyi kusafiri hadi Nairobi,” alisema Murkomen.

Mwaka huu tayari machifu 87 na manaibu machifu 58 wamepandishwa vyeo. Murkomen aliahidi watakaokamilisha mafunzo hayo watapandishwa vyeo “mara moja” kulingana na kanuni za Tume ya Huduma za Umma.

Mafunzo haya yanafanyika miezi michache baada ya serikali kurejesha polisi kwa machifu na maafisa wengine wa utawala wa serikali ya kitaifa kupitia kitengo kilichoanzishwa upya cha polisi cha maafisa wa utawala wa serikali ya kitaifa (NGAPU). Kitengo hiki kinashughulikia usalama mashinani na kinaripoti moja kwa moja kwa maafisa wa utawala kutoka kwa makamishna wa kaunti hadi kwa manaibu machifu.

Kitengo hicho tayari kimeajiri maafisa 6,000 kutoka Huduma ya Polisi wa Utawala na kuna mpango wa kuongeza idadi hadi maafisa 19,000 kwa awamu, kulingana na mahitaji ya kiusalama ya kila eneo.