Habari za Kitaifa

Magwanga amchoka Wanga, aamua kufanyia kazi nyumbani

Na COLLINS OMULO December 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

NAIBU Gavana wa Homa Bay, Oyugi Magwanga, amesema kuwa amechoshwa na hujuma na sasa atafanya kazi kutoka nyumbani kama mkakati wa kuepuka uhasama zaidi na bosi wake Gavana Gladys Wanga.

Bw Magwanga alisema kuhangaishwa kwake, hujuma usioisha, kusengenywa na kazi zake kusambaratishwa ni mambo ambayo yamekuwa yakimwaandama na hawezi sasa kuendelea kuyavumilia.

Alisema ni uhusiano mbaya kati yake na Bi Wanga ndio ulisababisha amuunge mkono mwaniaji huru Philip Aroko kwenye uchaguzi mdogo wa Kasipul mwezi uliopita.

Bi Wanga na viongozi wa ODM walimuunga mkono Boyd Were ambaye alishinda kiti hicho kilichokuwa kikishikiliwa na marehemu babake Charles Ong’ondo Were.

“Siwezi kufanya kazi bila bajeti na bado nitarajiwe nifaulu. Kuna kipindi kabati langu lilivunjwa afisini na hakuna hatua zilizochukuliwa. Hata kamera za CCTV zilifanya nishuku mambo zaidi,” akasema Bw Magwanga.

Kiongozi huyo alisimulia hali ambapo amekuwa akipitia dhuluma licha ya kwamba alighairi nia ya kuwania ugavana 2022 na kumuunga mkono Bi Wanga.

Marehemu Raila Odinga aliwapatanisha viongozi hao kuelekea mchujo wa ODM mnamo 2022 na Bw Magwanga akakubali kuwa mgombeaji mwenza wa Bi Wanga.

“Kwa miaka mitatu nimempa heshima sana kama bosi wangu licha ya kwamba namzidi umri. Hii ndiyo maana aliyekuwa waziri mkuu alitaka tufanye kazi pamoja, tungekuwa tumefikisha nchi hii mbali sana,” akasema.

Wiki jana afisi ya naibu huyo wa gavana katika makao makuu mpya ya Arujo zilifungwa huku akidai kulikuwa na wahuni ambao walikuwa wamepangwa wamvamie.

“Kufuli zilibadilishwa na wafanyakazi katika afisi yangu wakafungiwa nje. Niliandika barua ya malalamishi na hadi sasa sijajibiwa,” akaongeza.

Kwa sasa Bw Magwanga amesema hana nia ya kuingia katika afisi hiyo akitaja ukosefu wa usalama na pia kuvunjika kwa uhusiano kati yake na bosi wake.

Anasema kuwa sasa atakuwa akitumia mtandao na teknolojia kufanya kazi kutoka nyumbani kwake.

Bw Magwanga alifichua kwamba kulikuwa na makubaliano kuwa wagawane mamlaka kwa asilimia 60-40 huku akipata asilimia 40.

“Raila pia alipendekeza kuwa kama naibu gavana nipewe wizara na nikachagua ile ya kilimo,” akasema huku akisema Bi Wanga ameyakiuka makubaliano hayo.

Alifunguka zaidi na kusema wakati wa Kongamano la Ugatuzi 2025, Bi Wanga alikosa kumtambua na akatambua tu mume wake na Kiongozi wa Wengi kwenye Bunge la Kaunti, Richard Ogindo.

Pia alidai kuwa simu yake na ile ya wafanyakazi wake zinafuatiliwa na kuwa droni ilitumwa nyumbani kwake wakati wa uchaguzi mdogo wa Kasipul.