Magwanga sasa atangaza vita dhidi ya Wanga: ‘Ulipata ugavana sababu ya Raila’
GAVANA wa Homa Bay Gladys Wanga anakabiliwa na mtihani mkali kisiasa akisaka muhula wa pili 2027 baada ya Naibu Gavana Oyugi Magwanga kutangaza kuwa analenga kutwaa wadhifa huo mwaka ujao.
Bw Magwanga ameapa kwamba atafanya juu chini kuhakikisha kuwa anambwaga Bi Wanga ambaye pia ni mwenyekiti wa kitaifa wa ODM.
Alisema Bi Wanga alitumia ushawishi wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kuingia afisini mnamo 2022 kisha akawataliki baadhi watu waliomsaidia kutwaa ugavana.
Uhusiano kati ya Bi Wanga na Bw Magwanga ambao ulikuwa ukinawiri kwa sasa umeingia doa hasa kabla na baada ya uchaguzi mdogo wa Kasipul.
Bi Wanga anatarajiwa atautetea wadhifa wake 2027 japo kuna uvumi kuwa analengwa na Rais William Ruto ili awe mgombeaji mwenza wake.
Hata hivyo, binafsi amekuwa akisema lengo lake ni kuhudumu kama gavana kwa miaka 10 ili atamatishe miradi ya maendeleo aliyowaahidi wakazi wa Homa Bay.
“Nitakuwa gavana wa Homa Bay kwa mihula miwili na hili litawezekana tu iwapo nitawafanyia walionichagua kazi. Utawala wangu una miradi mingi ya kutekeleza ili kuyainua maisha ya watu wetu,” akasema Bi Wanga.
Bw Magwanga hata hivyo amesema yuko tayari kupambana na Bi Wanga hasa ikizingatiwa Bw Odinga sasa hayuko kuamua mkondo wa siasa za Luo Nyanza.
Kwenye video ambayo imesambaa mitandaoni, Bw Magwanga anasema kuwa Bi Wanga hafai kuchaguliwa tena kwa kufanya makosa mengi afisini.
Pia alidai kuwa kuna wanasiasa wandani wa Bi Wanga ambao washaamua kumwondoa kama mgombeaji mwenza wake 2027 na sasa hana budi kuendea ugavana.
“Kuna wandani wake wanataka saa nisalie naye ilhali washapanga kuniondoa mnamo 2027. Ni wao walianzisha vita hivi na nitaendelea kupambana nao,” akasema Bw Magwanga.
Naibu huyo wa gavana alijiunga na mrengo wa Bi Wanga mnamo 2022 baada ya Raila kuwapatanisha.
Wakati huo wote walikuwa wakilenga ugavana akiwemo pia Waziri wa Fedha John Mbadi ambaye pia alijiondoa na kumuunga Bi Wanga kutokana na ushawishi wa Raila.
Wachanganuzi wa masuala ya kisiasa wanasema Homa Bay itashuhudia ushindani mkali ikizingatiwa kwamba Bi Wanga na Bw Magwanga wote wana wafuasi wengi.
“Nilikubali kufanya kazi naye baada ya Raila kutuma watu wazungumze nami. Mwanzoni tulikosana lakini baadaye tukaelewana kwa sababu alikuwa mkubwa wangu kisiasa.”
Naibu huyo wa gavana alisema kuwa kuelekea uchaguzi wa 2022 alikuwa na umaarufu wa kisiasa na hata kura za maoni zilionyesha angetwaa ugavana kirahisi.
Kwa hivyo, anadai Bi Wanga aliwahi ugavana kutokana na umaarufu wake na ndiye alikuwa akiwatuma watu kwake ili wazungumze naye.
Bw Magwanga hajaweza kutumia afisi yake tangu Desemba mwaka jana baada ya kuondolewa kama waziri na mwandani wake kufurushwa katika Baraza la Mawaziri.
Haya yote yalitokana na hatua yake ya kumuunga mkono Philip Aroko katika kinyangányiro cha uchaguzi mdogo wa Kasipul mnamo Novemba mwaka jana.