Mahakama yaagiza Sh13.4m za Mathe wa Ngara ziendee serikali
NA SAM KIPLAGAT
MAHAKAMA Kuu imetangaza Sh13.4 milioni zilizotwaliwa kutoka kwa mfanyabiashara, Nancy Indoveria Kigunzu, mnamo Agosti 2023, kama mapato ya uhalifu na kuamuru pesa hizo zichukuliwe na serikali.
Jaji wa Mahakama Kuu, Esther Maina alisema Bi Kigunzu, anayekabiliwa na mashtaka ya ulanguzi wa dawa za kulevya, alishindwa kueleza chanzo cha hela hizo au kufafanua sababu ya kuweka kiasi hicho kikubwa cha pesa ndani ya magunia badala ya benki ambapo zingekuwa zinamzalishia riba.
Jaji huyo alisema kuna ushahidi kwamba maafisa wa polisi walipata mihadarati makazini mwake iliyogunduliwa baadaye kuwa bangi na ambayo kuimiliki na ulanguzi wake ni hatia.
“Imethibitishwa vilevile kwamba polisi walipata watu watatu katika makao hayo katika hali inayoashiria ni wahusika waliokuwa wakitumiwa katika ulanguzi wa mihadarati hiyo,” alisema Jaji na kuongeza kuwa ushahidi kuhusu mshabaha wa matukio kuwa hela hizo zinahusiana moja kwa moja na uhalifu hata ingawa kitendo cha uhalifu huo kingali hakijabainishwa.
“Ingawa mlalamishi hahitajiki kuthibitisha kitendo cha hatia mahususi, inahitajika hata hivyo kuthibitisha uhusiano kati ya mali na kitendo kinachokiuka sheria au uhalifu.”
Jaji Maina alisema Shirika la Kurejesha Mali ya Wizi (ARA) lilisema pesa hizo ni lazima ziwe za wizi kwa sababu polisi walipata bangi nyumbani kwake walipofanya msako mnamo Agosti 15, 2023.
Alisema shirika hilo lilithibitisha kuwepo uhusiano kati ya hela hizo na kitendo cha uhalifu.
Korti ilielezwa kuwa maafisa kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) walivamia makazi ya mshukiwa na kuwakamata watu watatu wanaoaminika kuwa vibaraka, washiriki na jamaa zake wa karibu.
Walipata vilevile kilo 610 za bangi na baadaye washukiwa wakashtakiwa katika korti ya JKIA kuhusu ulanguzi wa mihadarati, kumiliki mali ya wazi na kula njama ya kutekeleza uhalifu.
ARA kupitia Bw Mohamed Adow ilisema uchaguzi umebainisha misingi thabiti ya kuamini hela hizo zilipatikana kupitia biashara haramu ya mihadarati hivyo basi ni mapato ya uhalifu.
Kupitia Danstan Omari, mshtakiwa alipinga kesi hiyo akihoji kuwa mashtaka dhidi yake hayajakamilishwa na kwamba kesi hiyo inanuiwa kumnyima haki ya kusikilizwa bila ubaguzi.