Habari za Kitaifa

Mahakama yaamuru kanda za CCTV zitolewe katika kesi ya Albert Ojwang

Na RICHARD MUNGUTI December 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAHAKAMA Kuu ya Kibera imeiagiza Mamlaka Huru ya Polisi (IPOA) iwape mawakili wanaomtetea aliyekuwa mkuu wa kituo cha Polisi cha Central, Samson Talam anayeshtakiwa kwa mauaji ya mwalimu na bloga Albert Ojwang nakala za video za CCTV kabla ya kesi kuanza kusikizwa.

Jaji anayesikiza kesi hiyo alifahamishwa na mawakili sita wakiongozwa na Danstan Omari kwamba IPOA haijawapa video za kamera za CCTV zilizonakiliwa usiku wa Juni 7/8, 2025, Ojwang alipouawa katika seli kwenye kituo cha Central.

Ikiamuru video hizo za CCTV zikabidhiwe Omari na wenzake, Jaji Diana Kavedza alisema ushahidi huo ni muhimu zaidi kwani “kila mmoja anataka kujua kilichojiri kabla ya Ojwang kuuawa”.

“Bila ya video hizo za CCTV, kesi hii haiwezi kutengewa siku za kusikizwa. Ninajua kila mmoja wenu anahitaji kujua kilichompata mwalimu Albert Ojwang,” akasema Jaji Kavedza.

Jaji huyo alisema mawakili wanahitaji muda wa kuona na kutafakari kilichojiri kabla ya kuanza tetezi zao.

Talaam ameshtakiwa pamoja na James Mukhwana, Peter Kimani, John Ngige Gitau, Jim Ambao na Brian Njue.

Washtakiwa katika kesi ya mauaji ya mwalimu na bloga Albert Ojwang. Picha|Billy Ogada

Wamekana kumuua Ojwang usiku wa Juni 7/8 2025 katika Kituo cha Polisi cha Central alipokuwa amezuiliwa kuhojiwa kwa tuhuma za kupeperusha habari za kufedhehesha Naibu Inspekta Jenerali, Eliud Langat katika mitandao ya kijamii.

Polisi walimtia nguvuni Albert kutoka nyumbani kwake Kaunti ya Homa Bay alipokuwa anajiandaa kula chakula cha mchana na mkewe na wazazi wake.

Makachero waliomtia nguvuni walimweleza alikuwa anahitajika Nairobi.

Baba yake alimwachilia mwanawe aandamane na polisi lakini usiku huo ndio aliuawa. Jaji anayesikiza kesi hiyo alisema inafaa ikamilishwe kwa muda mchache kwa vile ina umuhimu mkuu kwa umma.

Upande wa mashtaka ulisema kuwa utawaita mashahidi 28.

Hata hivyo jaji alimtaka mkurugenzi wa mashhtaka ya umma apunguze mashahidi hao akisema huenda kesi hiyo ikachukua muda wa miaka miwili kukamilika.

Pamoja na hayo Jaji huyo alisema anaweza kupokea ushahidi wa mashahidi watatu kila siku ikitiliwa maanani alipokea ushahidi wa watu 100 katika siku 22 kwenye kesi ya kutamausha na kushtusha ya Shakahola.

Jaji huyo alisema kesi hii dhidi ya Talaam na wenzake sio kubwa kiasi kwamba haiwezi kukamilika katika muda mchache.

Jaji Kavedza aliwatahadharisha mawakili na viongozi wa mashtaka atahitaji wajichukue vyema pasi kuharibu muda mwingi na madaha wanapouliza mashahidi maswali.

Jaji huyo alisema ataidhibiti kesi hiyo ipasavyo ili ikamilike katika muda mchache iwezekavyo.