Mahakama yafichua jinsi matatizo ya kiufundi yalizuia kesi za kumwokoa Gachagua
IDARA ya mahakama imefichua jinsi kosa la kiufundi lilivyochangia kuwazuia walalamishi kuwasilisha kesi yao aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua alipokuwa akifurushwa afisini mnamo Oktoba.
Ufichuzi huo umejiri karibu miezi mitatu tangu tukio hilo lililosababisha walalamishi watatu kumwandikia barua ya malalamishi, Msajili Mkuu Winfridah Mokaya na Jaji Mkuu Martha Koome.
Waliitisha majibu kuhusu kilichofanya mfumo wa kielektroniki kufeli hivyo kuwazuia kuwasilisha kesi iliyohusu kumtimua Bw Gachagua.
Kupitia barua yenye anwani, “kuvurugwa kwa uwasilishaji wa kesi nambari E568 ya 2024 kwa lengo la kushinda haki” iliyoandikwa Oktoba 30, 2024, watatu hao: Miruru Waweru, Andrew Njoroge na Mutonga Kamau, walisema walitilia shaka mfumo huo kufeli siku hiyo.
Nakala ilieleza kwa kina jinsi malipo yao kielektroniki yalivyorejeshwa Oktoba 18 saa tatu asubuhi.
Walalamishi hao waliuliza sababu ya mfumo wa kuwasilisha kesi kielekroniki ulifeli ghafla Oktoba 18, siku ile ile ambayo Bunge la Kitaifa lilipiga kura kuthibitisha Profesa Kithure Kindiki kama aliyeteuliwa na rais na kutwaa nafasi ya Bw Gachagua.
Kufeli kwa mfumo huo kuliambatana na kurejeshewa pesa walizolipa jambo lililozuia kesi kusonga mbele kortini jambo wanalosema lilihujumu juhudi zao za kusimamisha mchakato wa bunge.
Walalamishi wanasema hitilafu hizo za kiufundi “zilisababishwa kimaksudi kwa nia ya kushinda haki,” na kumzuia jaji kuangazia upya kesi hiyo kwa wakati unaofaa.
“Ni maoni yetu kuwa mifumo ilikumbwa na hitilafu kutokana na jaribio la kuzuia kimaksudi kesi yetu kufika mbele ya jaji kwa wakati ufaao ili kuathiri idhini ya kuendeleza vikao,” inasema nakala ya kesi.
Barua hiyo ilihoji ni vipi hatua ya kurejeshewa hela iliyohusisha kampuni ya mawasiliano ya Safaricom, korti na Kenya Commercial Bank (KCB) ingetekelezwa pasipo idhini ya aliyelipa, jambo walilosema lilikuwa kuzuia kimaksudi.
Baada ya kujaribu mara kadhaa kukamilisha malipo, mlalamishi Waweru anasema hatimaye aliwasiliana na maafisa wa kuhudumia wateja Safaricom waliomshauri kutumia mbinu mbadala ya malipo kupitia “334#.
Alifuata maagizo, akafanikiwa kulipa, lakini bado hayakujitokeza kwenye tovuti ya korti na baadaye akarejeshewa hela alizolipa kielektroniki.
Walalamishi hao walifafanua jinsi walivyojaribu tena kufanya malipo yayo hayo saa tatu na dakika ishirini asubuhi 9.20 lakini mfumo ukatoa risiti iliyowekwa muhuri wa s a dakika kumi baadaye, jambo walilodai “liliwazidia shaka.”
Akijibu masuala yaliyoulizwa na walalamishi wiki sita baadaye, Msajili Mkuu Mokaya alisema walifanya “uchunguzi wa kina” na kubaini kuwa matukio ya siku hiyo yalitokana na hitilafu ya kiufundi.
Alifafanua kuwa mfumo wa kuwasilisha kesi kielektroniki umejumuishwa na mfumo maalum wa kufuatilia kesi wa Idara ya Mahakama (ERP) unaoshughulikia michakato yote ya malipo ikiwemo risiti.
Mifumo hiyo mitatu, alileleza Bi Mokaya, pia imeunganishwa na tasnia za malipo kutoka nje kama vile KCB na M-pesa akisema ufanisi wa mchakato wa malipo unategemea mawasiliano baina ya mifumo husika bila kuingiliwa.
“Matokeo ya udadisi wetu yanaashiria kuwa, mnamo Oktoba 17 usiku, tasnia jumuishi inayotumiwa na KCB kuwasiliana na Idara ya Mahakama ilikumbwa na hitilafu ya kimitambo, hivyo kuzuia ERP yetu kupokea malipo.
“Kutokana na haya, malipo yote ya Mpesa yaliyofanywa wakati huo yalirejeshwa kwa sababu mfumo wetu haungeweza kupatikana kwa uidhinishaji,” alisema.