Habari za Kitaifa

Mahakama yamzima Toto kumchafulia Khalwale jina

February 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu imemzima mfanyabiashara Cleophas Shimanyula almaarufu ‘Toto’ kuchapisha katika mitandao ya kijamii habari za kumhusisha Seneta wa Kaunti ya Kakamega Boni Khalwale na kifo cha mfanyakazi wake Kizito Amukune Moi.

Na wakati huo huo, jaji Janet Mulwa ameagiza kesi hiyo isikilizwe na Mahakama Kuu ya Kakamega badala ya kusikilizwa na kuamuliwa katika Mahakama Kuu ya Nairobi.

Dkt Khalwale amemshtaki Toto kwa kumharibia jina pamoja na familia yake inayojumuisha mabibi wake watatu na watoto 17.

Anaomba mahakama iamuru Toto amlipe fidia ya Sh1.3 bilioni.

Dkt Khalwale anasema Toto alitoa madai ya uongo kwamba mwanasiasa huyo alimuua mfanyakazi wake ilhali aliaga dunia baada ya kujeruhiwa na fahali wake.

Katika kesi iliyowasilishwa na mawakili Danstan Omari na Shadrack Wambui, Dkt Khalwale, mabibi wake na watatu na watoto wao 17 wanaomba mahakama imwamuru mfanyabiashara huyo kuwafidia kitita hicho kikubwa cha noti.

Dkt Khalwale amekana kwamba alimuua mfanyakazi wake mnamo Januari 28, 2024.

Mwanasiasa huyo ameeleza mahakama kwambaToto alikataa kuomba msamaha na kufuta katika mitandao ya kijamii habari za uongo alizochapisha akimhusisha na kifo cha Kizito.

Kizito alishambuliwa na kuuawa na fahali wa Khalwale alipokuwa anamlisha zizini.

Mawakili Omari, Wambui na Aranga Omaiyo wamedokeza kwamba ripoti ya upasuaji uliofanywa na madaktari wane, imethibitisha kwamba Kizito aliaga dunia kutokana na majeraha ya kufumwa na fahali huyo kwa pembe zake.

Kizito alizikwa Februari 5, 2024.

Fahali aliyesababisha kifo cha mtunzaji huyo aliuawa kulingana na mila na desturi za jamii ya Waluhya.

Mahakama imeelezwa kwamba Toto alikataa kumuomba msamaha Dkt Khalwale na kumtaka wakutane kortini.

Katika kesi iliyowasilishwa kortini, Bw Omari anaomba mahakama imwamuru Toto akome kabisa kueneza uongo na kuchapisha habari za kumkejeli mteja wake na familia yake.

Seneta wa Kakamega Boni Khalwale (wa pili kulia) akiwa katika mahakama ya Milimani alipomshtaki mfanyabiashara Cleophas Shimanyula almaarufu ‘Toto’ kwa kumharibia jina akidai ndiye aliyemuua mfanyakazi wake–Kizito Amukune Moi–ilhali aliaga dunia baada kuumizwa na fahali wa mwanasiasa huyo. PICHA | RICHARD MUNGUTI

Kwenye kesi hiyo, Dkt Khalwale amesema mshtakiwa ameeneza habari ambazo hawezi kuthibitisha kuhusu.

Katika nakala za kesi alizowasilisha mahakama kuu ya Milimani, Dkt Khalwale amedokeza kwamba yeye pamoja na familia yake wamesononeshwa na habari hizo za uongo kuhusu kifo hicho cha Kizito.

“Licha ya kumsihi Toto afute madai hayo, ameendelea kuchapisha habari za kupotosha zaidi na kumfedhehesha Dkt Khalwale,” Bw Omari ameeleza katika kesi aliyoshtaki mahakamani.

Aidha, seneta Khalwale ameeleza kwamba habari hizo za uongo zimemdunisha na kumharibia sifa kama kiongozi wa kaunti ya Kakamega.

Wakati wa uchaguzi mkuu uliopita alichaguliwa kwa zaidi ya kura 249,000.

“Matusi dhidi ya Dkt Khalwale ni matusi dhidi ya wakazi wa kaunti yote ya Kakamega,” Bw Omari amesema.