Pigo kwa Ruto mahakama ikipiga breki amri ya kulipa karo kupitia e-Citizen
MAHAKAMA Kuu imesimamisha kwa muda amri ya Wizara ya Elimu ya kuhimiza malipo yote ya karo na ada zingine yafanywe kwenye mtandao wa e-Citizen.
Daktari mmoja kutoka Nakuru alienda kortini kupinga agizo la serikali kwa wazazi kulipia karo ya shule kupitia mtandao wa e-Citizen.
Katika kesi aliyowasilisha Mahakama Kuu ya Milimani, Dkt Magare Gikenyi alitaka amri hiyo ya serikali inayowashurutisha wazazi kulipa karo ya shule kielektoniki kupitia mtandao huo, ifutiliwe mbali.
Aidha, alipinga kuanzishwa kwa ada mpya ya Sh50 na utekelezaji wa akaunti moja.
Dkt Gikenyi alihoji kuwa, maagizo hayo hayana msingi kisheria na kikatiba kwa sababu umma haukushirikishwa.
“Miradi yote hii inayotajwa kama ya kuboresha utoaji huduma kupitia e-Citizen ilibuniwa bila kushirikisha umma kwa vyovyote vile. Ada mpya inayotozwa ya Sh50 iliafikiwa kwa njia tatanishi,” alisema.