Mahakama yapiga breki jopo la Ruto kuchunguza deni
MAHAKAMA Kuu jana, Jumatatu, Julai 8, 2024 ilisitisha kwa muda jopo huru ambalo liliteuliwa na Rais William Ruto wiki iliyopita kukagua kiwango cha deni la taifa.
Jaji Lawrence Mugambi alizuia jopo hilo huru kuanza kazi kutokana na kesi iliyowasilishwa na daktari wa upasuaji kutoka Kaunti ya Nakuru Dkt Magare Gikenyi na Eliud Matindi.
Kupitia notisi kwenye gazeti, Rais Ruto aliteua jopo hilo kufanya tathmini ya kina kuhusu deni la taifa na kuwasilisha ripoti yake baada ya miezi mitatu.
Kiongozi wa nchi alisema kuwa ukaguzi huo ulilenga kutoa mwanga kuhusu deni la taifa, jinsi ambavyo rasilimali za nchi zimetumika na kutoa pendekezo la kudhibiti deni la taifa.
Rais alisema analenga kufanya hayo yote ili kuwaondolea Wakenya na kizazi kijacho mzigo wa kulipa madeni mengi.
Dkt Gikenyi na Bw Matindi hata hivyo wamesema kuwa jukumu la jopo hilo ni la mkaguzi wa hesabu za serikali na kuundwa kwake ni kinyume cha Katiba ya nchi.
“Tukisubiri kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi, natoa amri ya muda kuwa jopo hilo lisitekeleze wajibu wake.
Pia nafuta kwa muda notisi ya gazeti ambayo ilichapishwa mnamo Julai 5,” akasema Jaji Mugambi.
Mahakama iliamrisha kuwa kesi hiyo itajwe mnamo Julai 23 ili atoe mwelekeo zaidi.
Jopo hilo lilikuwa liongozwe na Mwenyekiti Nancy Onyango akisaidiwa na Profesa Luis Franceschi.
Wanachama wengine walikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Nchini Faith Odhiambo, Rais wa Muungano wa Wahasibu nchini (ICPAK) Shammah Kiteme na Rais wa Chama cha Wahandisi Nchini (IEK) Vincent Kimosop.
Hata hivyo, Bi Odhiambo alikataa uteuzi huo akisema kubuniwa kwa jopo hilo ni kinyume cha sheria kwa sababu majukumu hayo ni ya mkaguzi wa fedha za serikali.
“Iwapo mahakama hii ya heshima haitazima jopo hili lililobuniwa na Rais, basi itakuwa ikienda kinyume na nguzo za uongozi wa kuridhisha,” akasema Dkt Gikenyi.