Mahakama yazuia kiti cha Monda kutangazwa wazi
NA WYCLIFFE NYABERI
MAHAKAMA Kuu imesimamisha mipango yoyote ya kukitangaza wazi kiti cha unaibu gavana wa Kisii kwenye Gazeti rasmi la Serikali hadi kesi iliyowasilishwa mbele yake iamuliwe.
Kesi hiyo iliyowasilishwa katika Mahakama ya Machakos, inahusisha Bw Jared Ratemo na Bunge la Seneti.
Licha ya kupata afueni hiyo, Jaji Francis Rayola Oliel alishauri kwamba kesi hiyo isikizwe mbele ya Mheshimiwa Jaji Eric Ogolla wa Mahakama Kuu ya Milimani mnamo Aprili 10, 2024.
“Baada ya kuzingatia maombi yaliyotajwa kortini bila Wakili wa mleta maombi, inaamriwa kuwa notisi ya maombi ya tarehe 20 Machi, 2024 inaibua mambo mazito na hivyo kuthibitishwa kuwa ya dharura. Hali ilivyo na kuruhusu mlalamishi kueleza masuala yaliyotolewa katika ombi hili, hakuna gazeti litakalotolewa kutangaza kiti cha naibu gavana wa kaunti ya Kisii kuwa wazi hadi tarehe hiyo,” Jaji Rayola alisema.
Mlalamishi wa kesi hiyo alielekezwa kuipa Seneti notisi hiyo ndani ya siku tatu. Nayo Seneti ilipewa siku saba kujipanga kuhusu kesi hiyo.
Jumatatu wiki hii, Dkt Monda alipeleka katika Mahakama Kuu ya Kisii na kuwasilisha kesi sawia kama hiyo lakini hakupewa maagizo yoyote.
Haya yalijiri saa chache baada ya gavana Simba Arati kumtaja Bw Elijah Julius Obebo, Mwenyekiti wa sasa wa Bodi ya Utumishi wa Umma (CPSB) naibu wake kufuatia kutimuliwa kwa Dkt Monda.
Uteuzi wa Bw Obebo uliwekwa wazi katika Bunge la Kaunti ya Kisii mnamo Jumatano alasiri na Spika Philip Nyanumba.
“Waheshimiwa madiwani, ninayo furaha kuwajulisha kwamba nimepata mawasiliano kutoka kwa Mheshimiwa, gavana wa Kaunti ya Kisii, Paul Simba Arati, kuhusu mteule wa nafasi ya naibu gavana. Huku akisubiri kuidhinishwa na bunge, amemteua Bw Elijah Obebo kwenye nafasi hiyo,” Spika Nyanumba alisema.
Naibu gavana mpya aliyeteuliwa hajulikani sana lakini ni mtumishi wa umma aliyestaafu kazini ambaye anatoka katika ukoo wa Abanyaribari sawa na Dkt Monda.
Bw Obebo alijulikana mnamo Novemba 2023, alipoapishwa kama mwenyekiti wa CPSB.
Dkt Monda alitimuliwa afisini wiki jana baada ya Seneti kuafiki mashtaka yote manne kama yalivyoletwa na Bunge la Kaunti ya Kisii.
Kiini cha tuhuma zilizompelekea Bw Monda kufungishwa virago ni rushwa ya Sh 800,000 kutoka kwa Denis Mokaya kwa ahadi kwamba atamsaidia apate kazi ya Umeneja wa Mauzo katika Kampuni ya Maji na Maji-taka ya Gusii (Gwasco) pamoja na kukamatwa na kuwekwa kizuizini kaka yake mwenyewe, Reuben Monda, kwa kukata miti katika ardhi ya familia yao.
Bw Mokaya hata hivyo hakuiona kazi hiyo.
Maseneta hao walipiga kura kwa wingi kuunga mkono mashtaka yote manne yaliyotolewa dhidi yake.
Hayo ni pamoja na ukiukaji mkubwa wa Katiba, matumizi mabaya ya afisi, utovu wa nidhamu uliokithiri na uhalifu chini ya sheria za kitaifa.