• Nairobi
  • Last Updated June 6th, 2024 7:48 PM
Mahasla wala hu’ mzigo mpya wa ushuru ukisukwa

Mahasla wala hu’ mzigo mpya wa ushuru ukisukwa

COLLINS OMULO  NA BENSON MATHEKA

WAKENYA wa mapato ya chini maarufu kama mahsla wanaendelea kuteseka huku serikali ya Kenya Kwanza waliyounga mkono kwa kuwaahidi maisha nafuu ikiwabebesha zigo la ushuru.

Serikali imependekeza nyongeza mpya ya ushuru kwa bidhaa za kimsingi kama mkate, hatua ambayo itawaumiza raia ambao tayari wanalemewa na gharama ya maisha.

Hii ni tofauti na manifesto  ya Rais William Ruto wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 ambayo aliahidi kupunguzia Wakenya gharama ya maisha.

Dkt Ruto aliitaja manifesto yake kama tiba ya hali ya kiuchumi ambayo alidai  mtangulizi wake Uhuru Kenyatta  aliwasababishia Wakenya na hasa wale wa mapato ya chini.

Hata hivyo, alipoingia mamlakani 2022, hali imekuwa kinyume na kila ahadi aliyotoa wakati wa kampeni ambazo ziliwapa matumaini Wakenya na mapato ya chini hasa vijana wasio na ajira, akina mama na wafanyabiashara wadogo.

Badala ya kupunguzia raia mzigo wa gharama ya maisha, serikali yake, kupitia Sheria ya Fedha ya 2023 ilifanya hali kuwa ngumu kwa kuanzisha aina mpya za ushuru kama vie kuongeza maradufu  ushuru wa   thamani kwa bidhaa  za petroli hadi asilimia 16 pamoja na kufutilia mbali ruzuku ya mafuta ya taa na dizeli.

Kilichoongezea wengi uchungu ni ushuru wa asilimia 1.5 kufadhili mpango wa nyumba za bei nafuu, makato ya asilimia 2.75 wa hazina ya bima ya hospitali, na asilimia tatu ya ushuru wa mauzo (mauzo ya jumla) kwa biashara ndogo ndogo.

Shirikisho la Wafanyakazi  Kenya( FKE )liliripoti Wakenya 70,000 walipoteza kazi mwaka wa kwanza wa urais wa Dkt Ruto nai zaidi wako katika hatari ya kupoteza ajira huku waajiri wakiwazia kupunguzwa wafanyakazi zaidi.

Shirikisho hilo lililaumuutekelezaji wa Sheria tata ya Fedha, 2023 kama chanzo cha masaibu hayo.

Licha ya kuonywa kuwa hatua hizo mpya za ushuru zingewaathiri sana Wakenya, ambao wanatatizika kujikimu kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha na ukosefu wa ajira, Rais Ruto amerejea tena na mapendekezo ya kuongeza ushuru, hatua ambayo inaweza kumtenga zaidi na Wakenya wanaohangaika.

Wakenya wanapambana na gharama ya juu ya maisha na ushuru mpya ambao umepunguza kiwango cha pesa  wanachopata huku wengi wakishindwa kulipa karo, kununua  chakula na kuweka akiba ya kustaafu.

Kulingana na Ripoti ya Uchumi ya Kenya ya 2023 ya Taasisi ya Utafiti na Uchambuzi wa Sera za Umma ya Kenya (Kippra), wafanyakazi wengi bado wanapata mishahara ya chini.

Utafiti wa Disemba 2023 uliofanywa na Tifa ulionyesha kuwa wafuasi wa Kenya Kwanza ndio waliokata tamaa zaidi na hali ilivyo nchini.

Licha ya hayo, serikali inalenga kuongeza ushuru zikiwemo ada za huduma za kutuma na kupokea pesa kwa njia ya simu kama vile M-Pesa na za kuhamisha fedha kutoka benki na vyama vya akiba na mikopo  kutoka asilimia 15 hadi 20.

Hii itaongeza gharama ya kutuma pesa kwa simu,  gharama ya muda wa maongezi na data pia itaongezeka. Wakenya wanaopata mapato kutokana na shughuli za kidijitali ikiwa ni pamoja na kuendesha teksi  wataanza kulipa ushuru wa huduma za kidijitali wa asilimia 1.5. Zaidi ya hayo, serikali pia inapendekeza kuanzisha ada tata kwa bidhaa mbalimbali kama vile simu za mkononi, TV na betri.

Waundaji wa maudhui ya kidijitali ni vijana ambao serikali iliahidi kuboresha maisha yao. Ongezeko la ushuru litakuwa na athari kubwa kwa maelfu ya vijana ambao kwa sasa wanapata riziki kupitia kazi za dijitali. Serikali pia inapendekeza kuongeza ushuru kwa shughuli za kamari na michezo ya bahati nasibu  kwa mwaka wa pili mfululizo kutoka asilimia 12.5 mwaka 2023 hadi asilimia 20.

Katika kuzidisha uchungu kwa mahsla, serikali pia inapendekeza mfumo wa ushuru wa  uagizaji wa pikipiki kutoka nje ya nchi, utakaoathiri bei za pikipiki.Sekta hii imewafaidi zaidi vijana wanaokabiliana na viwango vya juu vya ukosefu wa ajira ambao wamekubali kazi ya bodaboda kama chanzo cha ajira.

Pia kuna pendekezo la ushuru wa asilimia 16 kwa mkate,hatua ambayo itapelekea gharama ya bidhaa hiyo kuongezeka kwa angalau Sh10 kwa mkate wa gramu 400.

Mbali na kuongeza ushuru, Rais Ruto alinyamaza kwa muda mrefu huku mgomo wa madaktari ukiendelea kwa takriban miezi miwili huku mwananchi wa kawaida akiteseka kwa kukosa huduma za matibabu katika hospitali za umma.

Mgomo huo ulisababisha wagonjwa wengi kuachwa kutoka kwa vituo vya afya vya umma bila kutunzwa huku Wakenya wakishindwa kumudu huduma katika hospitali za kibinafsi.

Seneta wa Kakamega Boni Khalwale aliikashifu serikali kwa kukosa kushughulikia haraka malalamishi ya madaktari wanaoishi Wakenya wanaoteseka.

“Ninahuzunika sana ninaposikia sauti nyingi za upande wa wachache zikisukuma ajenda sahihi na wengi katika upande wa walio wengi wakitetea ajenda zisizo sahihi,” alisema Khalwale ambaye ni Kiongozi wa Wengi katika Seneti.

“Najiuliza ni nani aliyewaambia wabunge kuwa walichaguliwa Bungeni kuiunga mkono Serikali hata pale inapokosea katika sera yake? Ni jukumu letu kukosoa vikali sera ya serikali ili tuifanye kuwa bora zaidi,” aliongeza.

Huku Kenya ikiwa nchi inayotegemea  kilimo,  kuna  uwezekano wa wakulima kupata mavuno kidogo ambayo yataathiri maisha yao na utoshelevu wa chakula kufuatia kashfa ya mbolea feki.

  • Tags

You can share this post!

Raila sasa aitishwa CV kabla ya kuruhusiwa rasmi kugombea...

Wamatangi atikisa UDA kwa kufufua kauli ya “Mtu...

T L