Maisha Bila Raila: Maadhimisho ya miaka 20 ya ODM kuendelea jijini Mombasa
GAVANA wa Mombasa, Abdulswamad Nassir, wikendi alithibitisha kuwa maadhimisho ya miaka 20 ya ODM yataendelea jijini Mombasa licha ya mauti ya Kinara wa chama hicho Raila Odinga.
Akizungumza katika mazishi ya Raila, Bondo, Kaunti ya Siaya, Bw Nassir alisema hafla hiyo itatumika kumuenzi kiongozi huyo wa upinzani kutokana na juhudi zake za kupigania utawala bora na demokrasia.
“Bw Odinga aliniamini niwe mwenyeji wa hafla ya kuadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwa ODM. Hatutakuwa tukiadhimisha miaka 20 tu bali pia juhudi za kupigania demokrasia na utetezi wa haki uliokuwa ukiendeshwa na Raila,” akasema Bw Nassir.
Gavana huyo alisisitiza kuwa ODM lazima isalie imara katika kupigania haki, uwazi, uwajibikaji na haki za Wakenya kama tu alivyokuwa akifanya Bw Odinga.
“ODM lazima ipiganie haki za watu,” akasema Bw Nassir.
Katika mazishi hayo, gavana huyo aliandamana na madiwani, wawakilishi wadi na wajumbe wa chama kutoka Mombasa kumwomboleza ‘Baba’.
Bw Odinga alifariki mnamo Oktoba 15 akitibiwa nchini India. Mwili wake ulirejeshwa nchini siku iliyofuata na akazikwa Jumapili kulingana na mapenzi yake.
Maadhimisho ya miaka 20 ya uwepo wa ODM yalistahili kuandaliwa Oktoba 10 hadi Oktoba 12. Hata hivyo, yaliahirishwa ili kuruhusu maeneo mengine pia kuandaa sherehe hizo.
Bw Nassir alikumbuka jinsi alivyopokea simu kutoka kwa Bw Odinga na kumtaka afike Nairobi. Alikuwa na kikao na kiongozi huyo kisha hafla hiyo ikafutwa na kuahirishwa hadi mwezi ujao.
Chama kilitangaza kuwa maadhimisho hayo yataandaliwa kutoka Novemba 14 hadi 16. Tayari maadhimisho hayo yalikuwa yameandaliwa Busia, Wajir, Kisii na Narok.
Wakati wa mazishi ya Raila, Bw Nassir alitoa wito kwa viongozi wenzake waimarishe chama mashinani na kujiandaa kwa chaguzi ndogo zinazokuja mwezi ujao pamoja na kura ya 2027.
“Sote chamani tuende tufanye kampeni kuhakikisha kuwa tunashinda Ugenya, Kasipul na Magarini. Tutumie chaguzi hizi kupata ushindi ili kumuenzi Raila,” akasema Bw Nassir.
Gavana huyo pia alisema kuwa chama hicho kitaendelea kuwa ndani ya Serikali Jumuishi kwa sababu hivyo ndivyo Bw Odinga alitaka.
Alisema uamuzi wa kujiunga na serikali ulitokana na mazungumzo ya kina na mashauriano ambayo yaliidhinishwa na Raila mwenyewe.
“Tuliketi kwa saa kadhaa tukijiuliza tujiunge na serikali ya Ruto au la. Sote tuliamua kujiunga na Serikali Jumuishi,” akasema.
Bw Nassir alisikitika kuwa kujiondoa kwenye mpango wa sasa wa kufanya kazi na Rais kutakuwa ni kumsaliti Raila.
“Nataka nikuhakikishie kuwa hatukukusaliti ulipokuwa hai na hatutakusaliti ukiwa umeaga dunia. Tunaendelea kushirikiana na serikali ili kukuenzi na kutimiza malengo yako,” akasema gavana huyo anayehudumu muhula wake wa kwanza.