• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Majangili Kerio Valley wapata mbinu mpya ya kuhepa polisi

Majangili Kerio Valley wapata mbinu mpya ya kuhepa polisi

FLORAH KOECH na BARNABAS BII

KIKOSI cha jeshi (KDF) na walinda usalama wanaoendeleza operesheni ya ‘Maliza Uhalifu’ ukanda wa Kaskazini mwa Bonde la Ufa, wanakabiliwa na kibarua kigumu kutokana na kuchipuka tena kwa visa vya uvamizi eneo hilo.

Visa hivyo, vimechangia mauti ya watu 10 na zaidi kwa muda wa wiki moja iliyopita. Hapo awali, majangili walikuwa wakipanga mashambulizi na hata kuwatishia watu ambao walikuwa wakilengwa kisha kuiba mifugo.

Hata hivyo, sasa wamebadili mbinu kwa kufanya uvamizi wa kushtukiza na kukosa kuiba chochote. Hii ni mbinu mpya ya kuhakikisha kuwa wanawazidi mbinu maafisa wa usalama ambao wamekuwa wakiendesha operesheni katika ukanda huo kwa karibu mwaka mmoja sasa.

Kwenye uvamizi wa hivi punde, watu watatu kutoka familia moja walipigwa risasi na kufa papo hapo huku wengine wakipata majeraha mabaya katika Kaunti ndogo ya Baringo Kaskazini.

Katika kisa tofauti, mabalozi watatu wa amani waliuawa kwenye Kaunti ndogo ya Marakwet Mashariki, tukio ambalo limekuwa pigo kubwa sana kwa juhudi ambazo zimekuwa zikiendelea za kusaka amani.

Wanafamilia waliouawa walijumuisha mke na mume pamoja na mtoto wao mwenye umri wa miaka miwili. Mauaji hayo yalitokea kwenye barabara ya Yatya-Chemoe katika eneobunge la Baringo Kaskazini.

Walikuwa wameabiri pikipiki kutoka mji wa Marigat, Baringo Kusini wakielekea kijiji cha Chemoe kwa sherehe ya upashaji tohara. Ni wakati wa safari hiyo, ambapo walivamiwa na majangili kutoka eneobunge jirani la Tiaty kisha kupigwa risasi.

Waliouawa ni Victor Yego, 30, mkewe Valentine, 28 na mwanao mwenye umri wa miaka miwili. Abiria mwingine, mwanafunzi wa kidato cha tatu na watu wawili waliokuwa wakiendesha pikipiki nao walipata majeraha mabaya ya risasi.

“Waliouawa walikuwa wakielekea kwenye sherehe ya upashaji tohara walipovamiwa. Waliojeruhiwa wanapokea matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Baringo,” akasema Kamanda wa Polisi wa Baringo Julius Kiragu.

Inakisiwa kuwa uvamizi huo ulikuwa wa kulipiza kisasi kufuatia kuuawa kwa mchungaji wa mifugo kutoka jamii ya Pokot wiki iliyopita.

Uvamizi huo ulitokea siku nne tu baada ya mabalozi wanne wa amani akiwemo mwalimu wa shule ya msingi kutoka kijiji cha Endo, Marakwet Mashariki kuuawa na majangili. Inashukiwa majangili hao walitoka jamii jirani.

Kamanda wa Polisi wa Elgeyo-Marakwet Peter Mulinge alisema kuwa maafisa wa usalama wameongezwa katika Bonde la Kerio kutokana na mauaji ya mabalozi hao wa amani.

Mabalozi hao walikuwa wameenda kuwapokea mbuzi ambao walikuwa wameibwa lakini wakarejeshwa na jamii ya Pokot.

“Maafisa wa GSU, wale wa kupambana na wezi wa mifugo, polisi na wale wa kukabili uvamizi wa ghafla, wanawasaka wavamizi,” akaongeza Bw Mulinge.

Uvamizi katika Bonde la Kerio umesababisha vifo vya zaidi ya watu 300 na kuwalazimu wengine kutoroka makwao kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

  • Tags

You can share this post!

Bamburi Cement yatoa hakikisho la kuzuia mavumbi kufikia...

Amerix awatia kiburi wanaume wa Tanzania...

T L