• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Majangili waua msichana na kuiba mifugo Kamologon

Majangili waua msichana na kuiba mifugo Kamologon

NA OSCAR KAKAI

TAHARUKI imetanda kwenye mpaka wa kaunti za Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet baada ya majangili kuvamia kijiji cha Kamologon mnamo Jumatano jioni na kumuua msichana wa umri wa miaka saba kisha kutoweka na mifugo.

Msichana aliyeuawa alikuwa mmojawapo wa watoto waliokuwa wanaendelea na shughuli zao za kawaida.

Mwili wa marehemu Shirleen Juliasia umepelekwa katika mochari ya hospitali ya Kapenguria.

Majangili hao wanaoshukiwa kutoka kaunti jirani ya Elgeyo Marakwet hadi Pokot Magharibi waliiba idadi ya mifugo isiyojulikana lakini askari wa akiba waliitwaa na kuirejesha.

Maafisa wa kupambana na wizi wa mifugo wameambiwa wakae chonjo.

Akithibitisha tukio hilo, Kamishina wa Kaunti ya Pokot Magharibi Khaliff Abdulahi alisema kuwa wamewasiliana na wenzao wa kaunti ya Elgeyo Marakwet kuhakikisha kuwa waliohusika na mauaji hayo wanakamatwa.

Eneo la Kamologon ambalo linapatikana Pokot ya Kati na Pokot Kusini, ni eneo la maficho ya majangili ambao hutekeleza mashambulio ya mara kwa mara.

Tangu mwaka 2024 uanze mashambulio yalikuwa yamepungua katika eneo hilo.

Viongozi wa eneo hilo wameshutumu vikali mauaji hayo na wizi wa mifugo na kutaka serikali kuimarisha barabara za kutumika na vikosi vya walinda usalama katika eneo hilo.

“Lazima upitie eneo la Pokot Kusini ndiposa ufike Kamologon. Tunataka Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki kuzuru eneo hilo Kamologon. Serikali imejaribu kufungua barabara lakini tunambia serikali kuu kutenga fedha nyingi za kufungua barabara ya Tapach-Kamelei-Rawal-Kamologon–Chepkoko,” anasema Seneta wa kaunti ya Pokot Magharibi Julius Murgor.

Mwakilishi wa Wadi ya Tapach Samuel Timtim Korinyang anasema kuwa shambulio hilo lilikuwa limepangwa na maafisa wa usalama wanafaa kuwekwa katika maeneo ya  Kapushen na Kamologon.

Aidha aliitaka serikali kufungua barabara ya Kapyegoh, Tangul, Kaprech, Tengwes-Lomut.

“Wale ambao walikuwa wanajenga barabara hiyo walivamia. Hatuelewi nia ya majirani zetu,”  anasema.

Wakazi wanasema kuwa majangili wamepuuza mikakati ambazo zimeweka ma waziri wa usalama Kithure Kindiki kurejesha usalama eneo lenye utata la Kaskazini mwa Bonde la Ufa.

Veronica Nang’ole, mkazi anasema kuwa akina mama na watoto ndio wameathirka pakubwa.

“Tunahitaji madwa sababu tunalala kwenye msitu. Tunataka maafisa wa afya eneo hili. Wacha vijana waache ujangili . Ni vyema serikali kuendeleza oparesheni ya kuondoa silaha haramu kama ilivyofanya serikali ya  Uganda,” alisema.

Wakazi wa eneo hilo, wamelalamikia ongezeko la visa vya usalama katika eneo hilo.

James Kapel, mkazi aliitaka serikali kushirikiana na askari wa akiba kuimarisha usalama.

“Wapokot na wanarakwet ni watu moja na wameoana. Tunataka wakilishi wa wadi kutoka kaunti zote mbili pamoja na viongozi wa kidini  kukutana na kumaliza uhasama,” anasema.

Alitoa wito kwa vikosi vya usaama kurejesha mifugo ambao wameibiwa.

Wiki jana, majangili walivamia kijiji cha Sorewo katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet, kilomita mbili tu kutoka eneo la Sindar, pale ajali ya ndege ya kijeshi ilianguka na kusababisha kifo cha Mkuu wa Majeshi (CDF) Jenerali Francis Ogolla na wanajeshi wengine tisa mnamo Alhamisi wiki jana.

Majangili hao pia waliiba mifugo 15 lakini ikarejeshwa na maafisa wa usalama.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Mackenzie aomba sabuni ya kuoga na ruhusa ya kumuona mkewe...

Kwa Man Utd sherehe Liverpool ikirambwa

T L