• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 2:54 PM
Majaribio ya upanzi wa mahindi Galana-Kulalu yapata ufanisi mkubwa

Majaribio ya upanzi wa mahindi Galana-Kulalu yapata ufanisi mkubwa

KABUI MWANGI NA BRIAN GEORGE

KAMPUNI ya kibinafsi imetangaza mipango ya kuwekeza angalau dola milioni 80 (Sh13 bilioni) katika mradi wa kilimo cha unyunyizaji maji wa Galana-Kulalu, Kaunti ya Tana River.

Kampuni hiyo ya Selu Limited, mojawapo ya kampuni zinazowekeza katika mradi huo, imesema itawekeza kiasi hicho cha fedha katika miaka mitatu ijayo, kufuatia awamu ya majaribio iliyofaulu mwaka uliopita.

Kampuni hiyo imeeleza kuwa majaribio yalileta mavuno ya mahindi yaliyovunja rekodi ya hadi magunia 35 ya kilo 90 kwa ekari moja, ambayo ni ya juu zaidi kuwahi kurekodiwa Galana-Kulalu na sasa inalenga kupanua shughuli katika shamba hilo la ekari 20,000.

Selu imefichua kuwa imehitimisha awamu ya awali ya kilimo kwa ekari 500, iliyohusisha tathmini ya ufanisi wa kilimo kikubwa cha mahindi kibiashara katika shamba hilo linalomilikiwa na serikali lenye jumla ya ekari milioni 1.75.

“Mradi huo una uwezo mkubwa wa kuboresha uzalishaji wa chakula cha kutosha Kenya, ambapo ekari 20,000 za ardhi zimetengwa kwa ajili ya kilimo-biashara, na kiwango cha juu cha mazao kinaweza kuongeza uzalishaji wa mahindi wa kila mwaka nchini Kenya,” Bw Nicholas Ambanya, Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Selu Limited alisema.

Kampuni hiyo inatekeleza mradi huo chini ya mpango wa muungano unaojumuisha mashirika ya LEAF Africa, Campo-Brazil na BrazAfric Group ambayo ilitoa utaalamu juu ya usimamizi wa mashamba makubwa ya kibiashara ya maeneo ya tropiki.

Kampuni hiyo ilisema uwekezaji huo, utaelekezwa katika kutekeleza unyunyizaji kikamilifu, kilimo bora na kuanzisha suluhisho la nishati mbadala katika juhudi za kuafikia uzalishaji wa chakula bila kuchafua mazingira kwa hewa ya kaboni. Harakati hizo zinalenga pia kubadilisha hali ya kijamii na kiuchumi ya jamii zinazopakana na eneo hilo.

Ustawishaji wa mradi wa Galana-Kulalu unafanywa kupitia ushirikiano wa sekta ya umma nakibinafsi na ni sehemu ya juhudi za serikali kufanya Kenya kuzalisha chakula cha ambacho kitatosheleza mahitaji ya umma.

“Katika awamu ya majaribio, Selu Limited ililenga kutumia mbinu za ubunifu kuwekeza na kubadilisha mradi wa unyunyizaji wa Galana Kulalu. Ilichukua hatua kadhaa muhimu ili kuhakikisha awamu ya maendeleo ya mradi itafanikiwa,” akasema.

Kampuni hiyo iliongeza kuwa, mbali na maendeleo ya kilimo, mradi wa Galana-Kulalu utabadilisha hali ya kijamii na mazingira ya jamii zinazoishi katika eneo hilo.

  • Tags

You can share this post!

SafeBoda yarejesha huduma zake nchini

Wafanyabiashara wanne washtakiwa kuiba dizeli ya Sh13.5m

T L