Tanzia: Mwalimu wa Gachagua aaga dunia
NA GEORGE MUNENE
KAUNTI ya Kirinyaga imetumbukia katika majonzi kufuatia kifo cha mwalimu mashuhuri Julius Kano Ndumbi ambaye alimshauri Naibu Rais Rigathi Gachagua enzi za ujana wake.
Akiwa na umri wa miaka 75, Mzee Ndumbi alipumzika alipokuwa akitibiwa katika Hospitali ya Mathari, Kaunti ya Nyeri ambako alikuwa amekimbizwa na kulazwa baada ya kuugua.
Kulingana na familia, Mzee Ndumbi, aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa shule ya Upili ya Wavulana ya Kianyaga alikuwa nyumbani kwake katika kijiji cha Giakuthu Kaunti ya Kirinyaga Jumamosi wiki jana alipoanza kuhisi vibaya.
Alikimbizwa katika hospitali haraka lakini akafariki wakati ambapo madaktari walikuwa wakimhudumia kuyaokoa maisha yake.
“Sasa tunaomboleza kifo cha Mzee Ndumbi wakati tunajiandaa kwa mazishi yake. Babangu alipelekwa hospitali ambako ilibainika kuwa ana matatizo ya moyo. Alipelekwa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) lakini akafariki dunia Jumatatu saa saba na dakika 40 usiku,” akasema Bw Peter Ngari, mtoto wa marehemu.
Marehemu Mzee Ndumbi alimfundisha Bw Gachagua kuanzia 1978 hadi 1982.
Alimshauri na kuhakikisha kuwa Bw Gachagua ambaye sasa ni wa pili katika ngazi ya uongozi wa Kenya, ana nidhamu.
Nyakati za nyuma Naibu Rais aliwahi kumrejelea Mzee Ndumbi kuwa mtu aliyemtia motisha na kumsaidia kufanikiwa maishani.
Katika mojawapo ya ziara zake Kirinyaga, Bw Gachagua alikumbuka vyema jinsi alivyorambishwa viboko vingi kutoka kwa Mzee Ndumbi.
“Ninakumbuka jinsi nilivyopigwa viboko vingi zaidi ya vile nilivyopaswa hivyo nikamwendea na kumuuliza kwa nini alinipa zaidi, kisha akajibu kuwa hayo yalikuwa kwa makosa nitakayofanya siku zijazo,” akasema Bw Gachagua alipokuwa ziarani Kianyaga, shule yake ya zamani.
Kabla ya kifo chake, Mzee Ndumbi alisema mara kwa mara kuwa nidhamu ni sifa aliyokuwa akiipenda miongoni mwa wanafunzi wake.
Aliamini kwamba kufundisha haikuwa kazi tu bali pia wito kutoka kwa Mungu ambao unapaswa kutekelezwa kwa dhati.
Zaidi ya hayo aliamini kwamba wanafunzi wote walikuwa sawa bila kujali hadhi ya familia walizotoka na wangeadhibiwa kulingana na makosa yao bila mapendeleo.
Wakati fulani, mzee huyo alimtaja Bw Gachagua kama mwanafunzi aliyebarikiwa kitaaluma, mwanasoka mwenye kipawa cha hali ya juu, mzungumzaji mwenye ufasaha, na mwanafunzi aliyekuwa na malengo makubwa na uchu wa kuyapata matokeo mazuri.
Na Bw Gachagua alipopanda ngazi hadi akawa Naibu Rais, Mzee Ndumbi alimtumia salamu za pongezi.
“Nina fahari kwamba umeenda juu sana kushikilia ofisi ya pili yenye nguvu zaidi katika ardhi hii,” alisema wakati wa uhai wake.
Marehemu Mzee Ndumbi aliwahi kuwa mkuu wa shule za upili za Kianyaga, Kangaru, Murang’a na Chuka ambapo aliacha alama na kumbukumbu isiyofutika.
Pia aliwahi kuwa Katibu Mtendaji wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) tawi la Kirinyaga.
Gavana Anne Waiguru alimrejelea kama mwalimu aliyejitolea na mchapakazi ambaye kifo chake kilikuwa pigo kubwa kwa kaunti nzima.
“Nimesikitishwa sana na kumpoteza Ndumbi ambaye alikuwa mwalimu mkuu, mtoa nidhamu, mshauri wa ajabu ambaye alikuwa na mchango mkubwa katika sekta ya elimu,” akasema Bi Waiguru katika rambirambi zake.