Habari za Kitaifa

Majonzi mwili wa mwanahabari ukisafirishwa kutoka Mombasa

Na MISHI GONGO October 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

HUZUNI ilitanda katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Jocham, mjini Mombasa, wakati familia ya aliyekuwa mwandishi wa habari Kimani Mbugua ikifanya maandalizi ya mwisho ya kusafirisha mwili wake kuelekea Nairobi.

Kulingana na babake marehemu Bw Kimathi Dedan, mwili utalazwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Montezuma jijini Nairobi, kabla ya mazishi yake yaliyopangwa kufanyika Jumanne nyumbani kwao Maragwa, Kaunti ya Kirinyaga.

Marehemu alikuwa na ugonjwa wa bipolar ambao uligunduliwa mwaka wa 2020.

Bw Kimathi, alisema kuwa mwanawe alikuwa amepambana na ugonjwa wa akili kwa muda mrefu na safari hiyo ilikuwa ngumu, lakini ilijaa matumaini kwani Kimani alijaribu kila mara kuyajenga upya maisha yake.

“Mwana wetu Kimani alianza kupata matatizo ya akili mwaka 2020. Aligunduliwa kuwa na bipolar. Ilikuwa safari ngumu sana,” alisema Bw Kimathi alipokuwa akizungumza na wanahabari nje ya chumba cha kuhifadhia maiti cha Jocham, wakati familia ikijiandaa kupeleka mwili katika uwanja wa ndege.

Kimani, ambaye aliwahi kufanya kazi kama mwandishi wa habari, alijitoa uhai mnamo Oktoba 14 usiku, na habari za kifo chake zikafahamika siku moja baadaye.

Kulingana na familia, matatizo ya Kimani ya afya ya akili yalianza mwaka 2020, ambapo alilazwa katika taasisi ya afya ya akili mjini Mombasa kwa mwaka mmoja.

Baada ya kupata nafuu, aliruhusiwa kuondoka, lakini miezi miwili baadaye hali yake ilijirudia tena na kulazimika kulazwa mapema mwaka huu.

“Safari hii alikuwa amekaa katika taasisi hiyo kwa miezi saba.Hatulaumu taasisi kwa kifo chake.Walijitahidi kumsaidia mwana wetu kwa kadri ya uwezo wao,” alisema Bw Kimathi.

Baba huyo alisema maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) walithibitisha video ya CCTV iliyomuonyesha mwanawe akijitoa uhai.

“Ilikuwa vigumu sana kutazama, lakini angalau ilitupa utulivu wa moyo.Aliniachia barua iliyosema, ‘Baba, nimechoka. Nimeamua kupumzika.’ Tulikuwa tunawasiliana mara kwa mara. Aliniambia, ‘Baba, nikistawi nitarejea katika uanahabari na kuwa bora zaidi,” alisema kwa huzuni.

Bw Kimathi alimtaja marehemu mwanawe kama kijana mwenye kipaji kikubwa na ubunifu aliyekuwa na ndoto ya kurejelea taaluma yake ya uanahabari.

“Ni pigo kubwa kwetu kama familia, si kwa sababu ya pesa, bali kwa sababu ya kipaji tulichopoteza. Pesa si kitu; kinachouma ni kupoteza mtoto mwenye kipawa,” alisema kwa majonzi.

Mwenyekiti wa Women Empowerment for Mental Health and Rehabilitation Centre, Bi Amina Abdallah, alisema marehemu Kimani alipelekwa katika kituo hicho kwa mara ya kwanza na aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko mwaka 2020.

“Alikuwa nasi kwa mwaka mmoja na aliachiliwa baada ya kuonyesha maendeleo makubwa.Lakini baada ya miezi miwili, hali yake ilirudi tena, huenda kwa sababu hakufuata maagizo ya kutumia dawa. Aliporejea safari ya pili, hali yake ilikuwa mbaya zaidi,” alisema.

Bi Abdallah alimwelezea Kimani kama mtu mwenye kipaji kikubwa.

“Alikuwa na nia ya kupata nafuu kwa sababu kila mara alikuwa akiomba kalamu, karatasi au kompyuta ndogo ili aandike,” alieleza.

Aliongeza kuwa marehemu alimwambia kwamba alijikuta amedhulumiwa pesa, jambo lililochochea hasira na huenda likasababisha kurudia kwa hali yake.

“Aliniambia alikuwa amekasirika kwa sababu mtu alimlaghai pesa zake. Nilimshauri kwamba tutashughulikia jambo hilo baada ya kupata nafuu,” alisema.

Bi Abdallah alisema unyanyapaa katika jamii ni changamoto kubwa inayowafanya wagonjwa wengi kushindwa kupona.

“Kwa mtu aliyewahi kuwa mwandishi anayeheshimika, ilikuwa vigumu kwake kukubali hali aliyokuwa nayo. Mara nyingi alihisi watu wanamdharau,” alisema.

“Unyanyapaa huwavunja moyo wagonjwa wengi kwa sababu huhisi wamekataliwa na jamii.”

Alizitaka familia na jamii kwa jumla kuwa na huruma na kuwasaidia wanaopambana na matatizo ya akili badala ya kuwahukumu.

“Ugonjwa wa akili ni kama magonjwa mengine unahitaji matunzo, kueleweka na subira. Wagonjwa wanapohisi wametengwa, hupoteza matumaini ya kuendelea kupigana,” alisema.

Familia ya Kimani ilitoa wito wa kuimarishwa kwa huduma za afya ya akili nchini ili kuzuia visa kama hivyo kutokea tena.

Mwili wa marehemu Kimani Mbugua unatarajiwa kuzikwa Jumanne nyumbani kwao Kirinyaga.

Kwa familia ya Kimathi, maumivu ya kumpoteza mtoto aliyewahi kuangaza vyumba vya habari bado ni makali, lakini wanapata faraja kwamba sasa amepumzika kutokana na mateso aliyokuwa akipitia.