Habari za Kitaifa

MAJOPO YA KUTAFUNA: Kamati 10 ndani ya miaka 3 ila matunda nadra kuonekana

Na COLLINS OMULO September 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto amegeuka gwiji wa kubuni majopokazi tangu achukue usukani huku mamilioni ya pesa za Wakenya yakitumika kufanikisha shughuli za asasi hizo ambazo manufaa yazo hayaonekani.

Tangu alipoingia mamlakani Septemba 13, 2022, Dkt Ruto amebuni zaidi ya majopokazi 10 baadhi yayo yakizimwa na mahamaka kwa kukiuka Katiba huku mapendekezo ya mengineyo yakikosa kutekelezwa.

Mfano ni jopokazi la hivi punde la kuendesha shughuli ya kutathmini ulipaji fidia kwa waathiriwa wa maandamanano ya kukosoa serikali, ambalo mahakama kuu ililipiga breki jana hadi kesi iliyowasilishwa kupinga kuundwa kwake itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Jopo hilo chini ya uenyekiti wa Mshauri wa Rais Ruto kuhusu Masuala ya Kisheria Prof Makau Mutua akisaidiana na mwenyekiti wa Chama cha Mawakili nchini (LSK), Faith Odhiambo lilipewa siku 120 kuchunguza, kuratibu na kutambua watakaolipwa fidia hiyo.

Wakosoaji wanasema pesa za umma zinatumika bila manufaa yoyote katika ufadhili wa shughuli za majopokazi hayo yanayoishia kutekeleza majukumu ya taasisi zilizoko za serikali.

Licha ya pingamizi za kuundwa kwa jopo la Prof Mutua, lililotwikwa majukumu yanayopaswa kutekelezwa na Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Kibinadamu (KNCHR), baadaye Rais Ruto aliunda kamati ya kiufundi ya kulainisha sekta ya michezo.

Kamati hiyo iliundwa mnamo Septemba 3, wiki moja baada ya kuapishwa rasmi kwa wanachama wa jopo la Prof Mutua mnamo Agosti 25, 2025.

Gharama ya jopokazi nchini Kenya hutofautiana kulingana na muda wake, idadi ya wanachama na mahitaji mahsusi.

Kimsingi, gharama inajumuisha marupurupu yanayolipwa wanachama, gharama ya sekretariati na gharama nyingine za ziada.

Gharama za utendakazi zinazoweza kujumuisha zile za kuandaa mikutano, usafiri wa wanachama, ukusanyaji wa data na mahitaji ya ziada kama vile ukodishaji wa washauri na uendeshaji wa utafiti.

Taarifa iliyotolewa na Tume ya Kutathmini Mishahara (SRC) kuhusu ulipaji wa marupurupu katika utumishi wa umma imeainisha marupurupu ya wanachama wa majopokazi.

Kulingana na mwongozo wa SRC, mwenyekiti wa jopokazi, ambaye ni mtumishi wa umma anafaa kulipwa marupurupu ya Sh5,000 kila siku, wanachama (Sh4,000), wafanyakazi wa sekretariati (Sh2,000) huku madereva na wasaidizi wakilipwa Sh1,000 kila siku.

Lakini kwa wanachama kutoka sekta ya kibinafsi, marupurupu huwa ni juu kwani mwenyeketi hupokea Sh15,000 kila siku, naibu mwenyekiti 12,000, wanachama, makatibu na wanasheria wasaidizi nao hulipwa marupurupu ya Sh10,000.

Watafiti, washauri wa kisheria, maafisa wasimamizi, washirikishi na wakuu wa usalama wanalipwa Sh4,000 kila siku.

Mahasibu, wachanganuzi wa data na maafisa wa ununuzi hulipwa Sh3,000 huku makarani na wakalimani wakilipwa Sh2,500. Nao madereva hulipwa Sh2,00 huku tarishi wakilipwa Sh1,800.

Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (NADCO) iliyoundwa na Rais Ruto na Kiongozi wa ODM Raila Odinga mnamo Julai 2023 iliitisha kitita cha Sh106 milioni kuendesha shughuli zake.

Kulingana na stakabadhi zilizoonekana na Taifa Leo wakati huo, wenyekiti wenza wa kamati hiyo; Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na kiongozi wa Wengi Bungeni, Kimani Ichung’wah walikuwa wakipokea Sh50,000 kwa kila kikao.

Nao wanachama wengine walioteuliwa kutoka sekta ya kibinafsi walikuwa wakitia kibindoni Sh25,000 kwa kila kikao.

Majopo mengine ambayo Rais Ruto ameunda ni lile la kuchunguza mauaji ya wanawake lililoongozwa na aliyekuwa Naibu Jaji Mkuu Nancy Barasa.

Jopo la kuchunguza mfumo wa elimu nchini lililoongozwa na aliyekuwa Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Moi Prof Raphael Munavu, lile la kuchunguza mauaji ya Shakahola na mambo ya kidini ni miongoni mwa mengine mengi yaliyobuniwa.

Majopo zaidi: Septemba 3, 2025: Kamati ya Kunyoosha Sekta ya Michezo; Septemba 2022: Jopo la kuchunguza Dhuluma za Kijinsia na Mauaji ya Wanawake (wanajopo 34); Februari 2023: Jopokazi la Kitaifa la Bahati-Nasibu; Mei 2024: Jopokazi la Kuifanya Kenya Maskani ya Chimbuko la Binadamu; Julai 2024: Jopokazi la Nguvukazi katika Sekta ya Afya (20); Desemba 2024: Jopokazi la Kushughulikia Hali ya Biashara Kuhamishwa Kenya (10).