Makamanda wa Mackenzie walimsaidia kutekeleza mauaji Shakahola
Kwa karibu miaka mitatu kuanzia mwishoni mwa 2019, mamia ya watu, wakiwemo watoto, walivutwa katika Msitu wa Shakahola, Kilifi, wakiamini wanaelekea kwenye maficho ya kiroho. Badala yake, eneo hilo liligeuka kuwa makaburi ya halaiki.
Kiini cha mkasa huo alikuwa mhubiri Paul Nthenge Mackenzie, ambaye mafundisho yake yaliwashawishi wafuasi kuacha makazi, kazi na maisha yao ya kawaida ili kujiandaa kwa kile alichodai kuwa ni mwito wa Mungu.
Lakini Mackenzie hakutekeleza mpango huo peke yake. Alikuwa na mtandao wa wafuasi aliowaamini ambao waliwatafuta waumini, kuratibu safari zao hadi msituni na kuhakikisha maagizo yake yanafuatwa.
Siku ya Ijumaa, Mackenzie alihukumiwa kifungo cha miaka 200 gerezani huku washirika wake wakipewa vifungo vya kati ya miaka 140 na 160.
Ushahidi uliowasilishwa mahakamani, ukiwemo ujumbe wa simu, rekodi za sauti na maelezo ya mashahidi, ulifichua jinsi mtandao huo ulivyofanya kazi. Ulionyesha jinsi jamii hiyo ilivyotawaliwa kwa hofu, maagizo ya kidini na vikwazo vilivyowazuia waumini kuondoka au kupata msaada.
Maafisa wa upelelezi walipata zaidi ya kurasa 74,000 za mazungumzo ya WhatsApp kutoka kwa simu za Mackenzie. Inspekta Mkuu wa Polisi Joseph Kolum, mtaalamu wa uchunguzi wa kidijitali wa DCI, alieleza kuwa jumbe hizo zilianza Septemba 2020 na zilihusu kufunga, mwisho wa dunia na maandalizi ya kurejea kwa Yesu Kristo.
“Data ilionyesha mazungumzo ya mara kwa mara kuhusu kufunga, Mpinga Kristo, Mpango Mpya wa Dunia na nambari 666,” Kolum aliambia mahakama.
Mackenzie aliwaonya wafuasi wake kuwa nguvu za kishetani zilikuwa zimepenya katika taasisi zenye mamlaka duniani. Aliwataka kuondoka katika makanisa na makazi yao na kuelekea msituni, akidai huko ndiko kulikokuwa na usalama wa kiroho.
Alisema: “Kanisa haliko tena majumbani mwenu; liko msituni.”
Pia aliwashawishi wazazi kuwatoa watoto shule na kukataa matibabu hospitalini. Wanawake walikatazwa kusuka nywele na kuvaa mapambo. Hata mfumo wa Huduma Namba ulietajwa kuwa kuwa alama shetani.
Hata hivyo, waumini hawakuvutiwa na mafundisho pekee. Wengine walivutiwa na ahadi ya kupata mashamba na kujenga makazi yao. George Mwaura, aliyeshiriki katika mipango ya ardhi, alieleza mahakama jinsi viwanja vilivyotolewa kwa waliohamia Shakahola.
Enos Amanya alisema eneo hilo liliwasilishwa kama kimbilio la waliochaguliwa na Mungu. Baadhi ya waumini waliuza mali na kutumia akiba zao kununua ardhi, wakiamini wangeishi huko wakisubiri kurudi kwa Yesu.
Ndani ya msitu, Mackenzie aligawa makazi hayo katika vijiji 12 vyenye majina ya kibiblia, kila kimoja kikiwa na kiongozi wake. Makamanda wake walihakikisha maagizo ya kufunga yalifuatwa, watu hawatoroki na waliojaribu kusaidia wengine walizuiwa.
Naibu wake, Smart Deri Mwakalama, alisaidia kusafirisha waumini, kusambaza maagizo, kuwakamata waliokuwa wakitoroka na kusimamia mazishi.
Stephen Sanga Muye, mkuu wa usalama, alihusika katika kushambulia mashahidi, kuchimba makaburi na kuzika upya watoto wa afisa wa GSU Isaac Ngala, ambaye pia alifariki katika mkasa huo.
Alex Munangwe Odari aliwakamata waliokuwa wakitoroka na kulinda maeneo ya kufungia watu kwa kutumia marungu na mapanga. Wakati wa operesheni za uokoaji, walinzi wa Mackenzie waliwahamisha waliofungwa ndani zaidi ya msitu ili kuwafanya waokoaji washindwe kuwafikia.
Mwinzi Kavenge alizuia juhudi za kuwafikia waumini waliokuwa wakifunga na kushambulia mashahidi kwa panga. Alfonze Chomba Eliud alijifanya afisa wa DCI ili kuwakatisha tamaa waliotaka kutoroka, huku pia akisafirisha miili hadi maeneo ya kuzikwa.
Mahakama pia ilielezwa jinsi miili ilivyozikwa usiku au alfajiri, makaburi yakatandazwa mchanga na mimea kupandwa juu yake ili kuficha ushahidi.
Mfumo huo ulihusisha hata familia. Amanya alikiri kufunga na kuwazika watoto wake sita. Mkewe, Ann Anyoso, aliwanyima watoto chakula na maji hadi wakafariki. Gilbert Kea Katana aligeuza nyumba kuwa maeneo ya kufungia watoto wake na kumshambulia mwanawe alipojaribu kutoroka.
Titus Munyao Musyoka alikuwa mlinzi, mchimbaji wa makaburi na msafirishaji wa miili. Mahakama ilielezwa kuwa alitazama chakula kikichukuliwa huku watoto wake saba wakifariki.
Wengine waliokuwa na majukumu ni pamoja na mchungaji Lucas Owino Ogola, aliyesaidia kuchimba makaburi ya watoto, na Michael Mweri Baya, aliyesambaza mafundisho ya Mackenzie na kuchimba makaburi.
Ushahidi huo ulionyesha kuwa Shakahola haikuwa tu jamii ya watu walioamini mafundisho ya mhubiri mmoja. Ilikuwa mfumo wenye viongozi, walinzi na wafuasi waliotekeleza maagizo, kuzuia waliotaka kuondoka na kuficha vifo.
Mackenzie alisingizia dini kuhalalisha mateso hayo, lakini washirika wake walisaidia kuhakikisha maagizo hayo yanatekelezwa hadi kusababisha vifo vya watu wengi.