Makamu Chansela wa Chuo cha Kenyatta aenda likizo ya muda usiojulikana
NA LABAAN SHABAAN
MAKAMU Chansela (VC) wa Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU), Prof Paul Wainaina ameelekea likizo ya muda usiojulikana.
Naibu Makamu Chansela wa Masuala ya Elimu, Prof Waceke Wanjohi atakuwa Kaimu VC kuanzia Aprili 15, 2024.
Kupitia notisi kwa wafanyakazi wa chuo, Prof Wainaina alitangaza hatua yake ya kuenda mapumziko.
Prof Wainaina, hata hivyo, hakuelezea likizo hiyo itachukua muda gani.
“Nikiwa mapumzikoni, Baraza la Chuo limemteua Prof Waceke Wanjohi kuwa Kaimu Makamu Chansela wa Chuo kuanzia Aprili 15, 2024,” aliandika Prof Wainaina.
Notisi hiyo iliendelea kuomba jumuiya ya chuo kushirikiana na kaimu mshikilizi huyo wa uongozi.
Prof Waceke anashika hatamu za uongozi kwa mara ya pili baada ya mgogoro kuibuka mwaka wa 2022 punde kabla ya uchaguzi mkuu nchini.
Prof Wainaina aliingia katika mzozo na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta kuhusiana na matumizi ya ardhi ya chuo.
Makamu Chansela alitakiwa na serikali kutoa sehemu ya ardhi ya KU ili itumiwe kujenga Kituo cha Kikanda cha Shirika la Afya Duniani (WHO).
Alipodinda kuachilia shamba la ekari 200, serikali ilimtimua na kubadilisha uongozi wa baraza la chuo.
Hapo ndipo Prof Waceke Wanjohi aliteuliwa kuwa Kaimu VC kabla ya Prof Wainaina kurejeshwa baada ya Rais William Ruto kuwa Rais wa tano wa Jamhuri ya Kenya mwaka wa 2022.