Habari za Kitaifa

Makanisa ya Kipentekoste yataka Bunge itunge sheria kuthibiti vyuo vya thiolojia

Na SAMWEL OWINO October 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Vyama vya makanisa ya Kipentekoste sasa vinataka Bunge litunge sheria itakayodhibiti ongezeko la kiholela la vyuo vya thiolojia nchini.

Kiini cha hoja ya ombi lililowasilishwa katika Bunge la Kitaifa ni kwamba wingi wa vyuo vya theolojia umesababisha kuwa na wachungaji wasiohitimu ipaswavyo na kukomaa kikamilifu, hali ambayo inatishia huduma ya injili.

Katika ombi lake, Pasta Josiah Njiru ambaye ni mwenyekiti wa Muungano wa Taasisi za Mafunzo ya Kiufundi za Kipentekoste nchini Kenya, unaodai kuwa na zaidi ya vyuo 200 vya Biblia kote nchini, anasema ongezeko la vyuo vya thiolojia limechangia kutolewa kwa shahada zenye utata kwa wachungaji ambao hawana uelewa wa kina wa injili.

Mchungaji Njiru anabainisha kuwa katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la vyuo vya Biblia, shule za thiolojia na majukwaa ya mafunzo ya injili mtandaoni, nyingi bila mwongozo au mamlaka ya askofu.

Anasema hali hiyo imechangia changamoto kama ukosefu wa mtaala bora, taasisi zisizo na ithibati, na shahada zisizothibitishwa, hali inayosababisha mkanganyiko na ukosefu wa maandalizi ya wachungaji katika makanisa mbalimbali.

“Kukosekana kwa mfumo wa udhibiti wa mafunzo ya thiolojia kumekuwa na athari kwa uaminifu, ubora wa mafunzo na uadilifu katika huduma za kanisa,” inasema sehemu ya ombi hilo.

Pasta Njiru anasema kuwa sheria zilizopo kama vile Sheria ya TVET, Sheria ya Vyuo Vikuu na Sheria ya Mfumo wa Kitaifa wa Kuhitimu(KNQF) zinashughulikia elimu ya kawaida pekee na hazitoi mwongozo kwa elimu ya kiroho au mafunzo ya kidini.

Kwa hivyo, anataka Bunge litunge sheria itakayoruhusu sekta ya makanisa ya Kipentekoste na Kiinjilisti kuanzisha mamlaka ya kujisimamia ili kudhibiti elimu ya theolojia.

Kwa mujibu wa ombi hilo, mamlaka hiyo itakuwa na jukumu la kuthibitisha vyuo vya thiolojia na mafundisho yake, kutambua mafunzo ya awali ya wahusika, na kuhakikisha mafundisho yanabaki ya kweli kulingana na mafundisho ya Biblia.

Ombi hilo limefufua upya mjadala kuhusu ikiwa makanisa na viongozi wa kidini wanapaswa kudhibitiwa na serikali au waongozwe na Roho Mtakatifu.

Mjadala huo uliigawanya Bunge, ambapo baadhi ya wabunge walisisitiza kuwa muda umefika wa kuweka sheria kali za kudhibiti utendakazi wa makanisa kwani kuwaacha waendeshe shughuli zao kiholela kumechangia kuporomoka kwa maadili ya jamii.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge walionya kuwa kudhibiti dini kunaweza kuwa na athari kubwa na hatari, na kwamba makanisa yaachwe yaendeshe shughuli zake kwa uongozi wa Mungu.

Mbunge wa Funyula, Dkt Wilberforce Oundo alisema alishangaa kwamba ombi kama hilo linaweza kuwasilishwa bungeni.

“Hili litakuwa ni kupoteza muda wa umma. Jamii ya kidini imekuwa ikipinga aina yoyote ya udhibiti kwa sababu wanataka uhuru wa kutoa mafundisho yao bila changamoto yoyote,” alisema Dkt Oundo.

Kamati ya Maombi ya Umma itachunguza ombi hilo na kuwasilisha ripoti yake kwa Bunge ndani ya siku 60.