• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Makatibu wa wizara waagizwa kubuni kamati za kupambana na ufisadi

Makatibu wa wizara waagizwa kubuni kamati za kupambana na ufisadi

NA CHARLES WASONGA

SIKU chache baada ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuanika uozo wa ufisadi serikalini, makatibu wa wizara (PSs) wameagizwa kubuni Kamati za Kupambana na Ufisadi (CPC) katika idara zote wanazozisimamia.

Agizo hilo lilitolewa baada ya mkutano wa Kamati ya Kitaifa ya Utekelezaji wa Maendeleo (NDIC) uliofanyika Ijumaa chini ya uenyekiti wa Mkuu wa Mawaziri na Waziri wa Masuala ya Kigeni Musalia Mudavadi.

“Idara zote za serikali kuu ziliamriwa kuanzisha Kamati za Kupambana na Ufisadi chini ya uenyekiti wa Makatibu wa Wizara. Kwa njia hii, serikali inalenga kuimarisha juhudi zake za kupambana na ufisadi,” ikasema ripoti ya NDIC iliyotumwa kwa vyombo vya habari baada ya mkutano uliofanyika katika afisi ya Bw Mudavadi iliyoko makao makuu ya Shirika la Reli Nchini (KRC).

Makatibu hao wa wizara walikumbushwa kuhusu wajibu wao kwa raia na kuhimizwa kuhakikisha kuwa ufisadi hauruhusiwi kupenya katika idara wanazozisimamia.

Makatibu wote 51 wanaosimamia idara mbalimbali katika wizara zote 22 za serikali ya Kenya Kwanza walihudhuria mkutano huo, kwa misingi kuwa wao pia ni wanachama wa kamati ya NDIC.

NDIC imetwikwa wajibu wa kusimamia utekelezaji wa mipango, sera na miradi yote ya Serikali ya Kitaifa.

Mwenyekiti wake ni Bw Mudavadi huku Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei akiwa naibu mwenyekiti.

Mnamo Machi 27, 2024, EACC ilitoa ripoti yake kuhusu visa vya ufisadi katika serikali kuu na serikali za kaunti ambapo ilibainika kuwa uovu umekithiri zaidi katika viwango hivyo vya serikali.

Wizara ya Usalama wa Ndani ndio iliyoorodheshwa kama iliyosheheni visa vingi zaidi vya raia kuitishwa hongo ili kupewa huduma mbalimbali.

Kulingana na ripoti hiyo, kima cha uitishwaji hongo katika wizara hiyo inayoongozwa na Waziri Kithure Kindiki ni asilimia 47.1 ikifuatwa Wizara ya Afya yake Susan Nakhumicha kwa asilimia 13.2.

Nayo Wizara ya Uchukuzi yake waziri Kipchumba Murkomen inashikilia nambari tatu kwa asilimia 5.8 ya visa vya raia kuitishwa hongo kwa huduma.

Asasi za serikali kuu ambazo ziliorodheshwa kama zilizosheheni visa vingi vya raia kuitishwa hongo kabla ya kupewa huduma ni Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama Barabarani (NTSA), Idara ya Mahakama, Idara ya Uhamiaji–sanasana kitengo cha utoaji pasipoti, Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa (Kebs), na Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) ambapo kitengo cha trafiki kiko juu.

Aidha, ripoti hiyo ya EACC ilibaini kuwa Wakenya hulipa kiasi cha wastani cha Sh163,000 kama hongo ili kupata ajira katika serikali ya kitaifa.

Aidha, kiwango cha hongo ambacho wao hutoa ili kupata huduma mbalimbali kimefikia Sh11,685 kwa wastani.

  • Tags

You can share this post!

Ndoa zasambaratika kwa vijana kutafuta ajira majuu –...

Mbolea feki: Linturi kuhojiwa na maseneta

T L