Habari za Kitaifa

Mali ya Didmus Barasa hatarini kupigwa mnada

Na MOSES NYAMORI November 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MALI ya Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa iko hatarini kupigwa mnada kwa kukosa kumlipa Katibu wa zamani na Balozi Patrick Wamoto jumla ya Sh8 milioni kwa kumharibia sifa.

Hakimu Mkazi wa Milimani S.K Onjoro mnamo Julai, alimpata Bw Barasa na hatia ya kutoa matamshi ya kumchafulia jina Bw Wamoto.

Kwenye amri ya mahakama, mbunge huyo aliamrishwa alipe pesa hizo na kumwomba msamaha Bw Wamoto kwenye redio inayotangaza kwa lugha ya mama ambako aliyatoa matamshi hayo miaka sita iliyopita.

“Didmus Wekesa Barasa aliamrishwa na mahakama hii mnamo 23/07/2025 kumlipa mlalamishi Sh8,047,021.98. Tunaamrisha mali yake itwaliwe iwapo atakosa kulipa hela hizo,” ikasema amri ya mahakama kwa kampuni ya mnada ya Fisra.

Bw Wamoto alienda mahakamani akilalamikia matamshi ya mbunge huyo kuwa ndiye aliwashawishi wenzake katika kamati ya mbunge kuidhinisha uteuzi wake kama kamishina wa Tume ya Uajiri wa Watumishi wa Umma (PSC).

Mahakama ilikubaliana na Bw Wamoto kuwa kauli hiyo ilikuwa na maana kuwa hakuwa amehitimu na kwamba alipata kazi hiyo kwa kusaidiwa.

“Kutokana na matamshi hayo, sifa za mlalamishi zilivunjwa na anastahili kufidiwa,” akasema hakimu huyo.

Balozi huyo wa zamani na baadaye Katibu wa kudumu katika Wizara ya Masuala ya Nje alisema alikuwa mtumishi wa umma ambaye alikuwa amehudumu kwa kipindi cha miaka 34.

Bw Wamoto alikuwa kamishina kwenye PSC wakati ambapo mbunge huyo aliyatoa madai hayo.

Wakati wa vikao vya kesi, Bw Barasa alikiri kwamba alihudhuria mahojiano katika kituo kimoja mnamo Oktoba 25, 2019 na kwamba sauti iliyonaswa ilikuwa yake.

Wakati wa kuhojiwa mahakamani, Bw Barasa alisema hakuwa na habari zozote kuhusu skendo ama rekodi ya uhalifu ya Bw Wamoto.

Mbunge huyo wa Kimilili alisema kuwa matamshi yake kwa lugha ya Kibukusu yalitokana na uvumi aliousikia kutoka kwa mbunge mwengine na kwamba yalifasiriwa vibaya.

Kwenye utetezi wake, alisema Bw Wamoto hakuharibiwa sifa au kuponzwa kivyovyote.

Hata hivyo, hakimu alisema matamshi hayo ambayo yalipeperushwa kwenye idhaa inayosikizwa sana, ilimsawiri Bw Wamoto vibaya na kumvunjia heshima katika jamii.

“Mlalamishi alisema alipokea simu nyingi kutoka kwa wasikilizaji kuhusu sifa zake,” akasema hakimu.

Aliongeza kuwa mienendo ya Bw Barasa ikiwemo kukataa kwake kuomba msamaha, kulionyesha kuwa matamshi aliyoyatoa kuhusu balozi huyo yalikuwa ya kweli.