Mama ashtakiwa kwa kula njama za kuua mfanyabiashara
MAMA alishtakiwa mnamo Jumatano, Agosti 21, 2024 kwa kula njama za kumuua mfanyabiashara Antony Maina Mutahi.
Awali, Winfred Wandia Kisau alikuwa amefikishwa kortini na polisi walioomba muda wa siku 21 kukamilisha mahojiano na uchunguzi dhidi yake.
Polisi walifichua kuwa mshtakiwa alishirikiana na mwanamke mwingine anayedaiwa alikosana na mlalamishi kabla ya njama za kumwangamiza zilipopangwa.
Kwa mujibu wa polisi, mshtakiwa aliombwa atafute muuaji alipwe Sh1 milioni na akikamilisha ‘mradi’ huo wa kumuua Maina, ataongezewa kitita cha Sh20 milioni.
Polisi walidai kwamba Wandia alimtafuta mtu kumuua Bw Maina.
Alikuwa ameahidi kumlipa Marvin Omondi Sh21 milioni akifaulu kumuua.
Lakini mpango huo ulitibuka Omondi alipomwendea Maina na kumsimulia na kumfichulia yote yaliyokuwa yanatokota.
Polisi walipokamilisha uchunguzi Jumatano, Agosti 21, 2024 walimfikisha Wandia kortini.
Mahakama iliombwa imwachilie kwa dhamana Wandia, huku wakili aliyemwakilisha akisimulia, “mshtakiwa alikuwa ameachiliwa na hakimu mkuu Bernard Ochoi kwa dhamana ya Sh200, 000.”
Wakili aliomba mahakama imwachilie mshtakiwa kwa dhamana sawa na hiyo.
Bi Wandia, hata hivyo, alikana kula njama za kutaka kumuua Maina Mutahi kati ya Julai 1 na Agosti 1, 2024 jijini Nairobi.
Alishtakiwa mbele ya hakimu mkuu Susan Shitubi.
Bi Shitubi aliombwa amwachilie Wandia kwa dhamana.
“Naomba hii mahakama imwachilie kwa dhamana. Mshtakiwa anaishi Mlolongo na hawezi kutoroka. Alikuwa nje kwa dhamana ya Sh300, 000 na amefika kortini kujibu mashtaka,” wakili aliyemwakilisha mshtakiwa aliambia korti.
Bi Shitubi alimwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya Sh300, 000 pesa tasilimu.
Kesi inayomkabili Wandia itatajwa tena Septemba 3, 2024.