Mama watoto wake wanne waangamizwa kwa kuchomwa katika mzozo wa mapenzi
Watu sita, akiwemo mama na watoto wake wanne kutoka Bulapesa, Isiolo, walifariki kwa kuchomeka hadi kutotambulika, huku nyumba mbili zikiteketezwa katika matukio mawili tofauti yaliyoacha wakazi wa eneo hilo katika mshangao na huzuni.
Msiba huo ulitokea Jumanne usiku moto ulipolipuka katika nyumba ya Bi Halima Warri, na kumchoma yeye pamoja na watoto wake wanne waliokuwa ndani ya nyumba hiyo.
Chifu Abdi Dida alisema kuwa juhudi za wakazi kuwaokoa ziligonga mwamba kutokana na upepo mkali uliosambaza moto kwa kasi, huku wakikosa zimamoto lililoweza kufika kusaidia kuzima moto huo.
“Kwa bahati mbaya, mama na watoto wake walifariki dunia katika tukio hilo. Hakukuwa na gari la zimamoto, na wakazi pia walishindwa kuuzima moto huo,” alisema Bw Dida.
Katika tukio la kusikitisha zaidi, wakazi wenye hasira walishambulia na kumuua mwanamke mmoja aliyeshukiwa kuanzisha moto huo, ikidaiwa kuwa ni kutokana na mzozo wa mapenzi.
“Nyumba ya mshukiwa pia ilichomwa na kuharibiwa kabisa. Tulipokea taarifa kuwa umati huo ulipanga kuwadhuru watoto wa mshukiwa waliokuwa shuleni. Tumepeleka polisi shuleni kuwalinda watoto hao, ambao pia watahifadhiwa mahali salama,” aliongeza chifu huyo.
Chifu Dida aliwataka wakazi kuepuka kuchukulia sheria mikononi na kuwahimiza kuishi kwa amani na maelewano.
Bw Omar Gabra, mkazi wa eneo hilo, alilaani matukio hayo na kuyataja kuwa “mambo ya ajabu na ya kusikitisha sana.”
“Tukitofautiana, ni muhimu tutafute suluhu kwa utulivu. Inasikitisha sana kuwa watu sita wameangamia kwa sababu ya mzozo. Hili ni jambo ambalo lingeweza kutatuliwa na wazee,” alisema Bw Gabra.
Mkazi mwingine, Bw Mohamed Tubi, alitaka uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo la uchomaji moto linalodaiwa kuwa la makusudi, ambalo liliangamiza familia nzima, na kumwacha mtoto mmoja tu aliyenusurika ambaye yuko katika shule ya upili.
“Tunaelewa kuwa marehemu alikuwa ameripoti vitisho dhidi ya maisha yake hapo awali. Polisi wanapaswa kuchunguza kwa undani ili kubaini ukweli wa kile kilichosababisha vifo vya mama huyo na watoto wake wasio na hatia,” alisema Bw Tubi.
Waathiriwa wote walizikwa Jumatano asubuhi kwa kuzingatia mila na taratibu za kiislamu.