• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Mamake Jowie: Nina imani mwanangu ataachiliwa huru

Mamake Jowie: Nina imani mwanangu ataachiliwa huru

NA WANDERI KAMAU

MAMAKE Joseph ‘Jowie’ Irungu mnamo Jumatano alieleza kutoridhishwa na uamuzi uliotolewa na Jaji Grace Nzioka, ambapo alimhukumu kifo mwanawe.

Akiwahutubia wanahabari nje ya mahakama jijini Nairobi, Bi Anastacia Thama alikosoa uamuzi huo, akisema anaamini kuwa mwanawe hakuwa na hatia yoyote na alihukumiwa isivyofaa.

Hata hivyo, alielezea imani yake kwamba watapata haki na hatimaye mwanawe ataachiliwa.

Akirejelea Biblia, alisema kuwa: “Mungu anayemtumikia atasaidia mwanangu kutoka nje ya gereza”.

“Ninaamini kuwa mwanangu hana makosa yoyote na hajamuua mtu yeyote. Naamini kuna Mungu anayempa mtu nafasi ya pili,” akasema Bi Thama.

“Mwanangu ni kama Yusufu katika Biblia ambaye aliteseka lakini Mungu akamsaidia. Ataachiliwa. Hiyo ndio sababu inanifanya kuwa na nguvu kwamba mwanangu ataachiliwa wakati ufaao utakapofika,” akaongeza.

Mamake Irungu alitoa kauli hiyo dakika chache baada ya mahakama kumhukumu kifo kutokana na mauaji ya Bi Monicah Kimani mnamo Septemba 2018.

Kwenye uamuzi wake, jaji Nzioka alisema ushahidi uliotolewa ulionyesha kuwa mshtakiwa alitekeleza mauaji hayo.

Miongoni mwa sababu ambazo jaji alizingatia katika kutoa uamuzi wake ni jinsi mauaji hayo yalivyotekelezwa, athari za kosa hilo na mienendo ya mshtakiwa.

Jowie alikuwa ameshtakiwa pamoja na mwanahabari Jacque Maribe ambaye baadaye alipatikana bila hatia.

Bi Maribe kwa sasa ni mkuu wa mawasiliano katika afisi ya Waziri wa Utumishi wa Umma Moses Kuria.

  • Tags

You can share this post!

Serikali yasutwa kwa kunyima vyombo vya habari matangazo ya...

Muigai wa Njoroge: Mwanamuziki anayesifika kwa nyimbo za...

T L