Mambo hayatakuwa rahisi, vijana wa Gen Z waonya Ruto, wabunge
MAANDAMANO ya vijana wanaopinga mapendekezo ya ushuru kwenye Mswada wa Fedha 2024 huenda yakavuruga ndoto ya Rais William Ruto na wabunge kuchaguliwa tena 2027.
Kwa kutumia mitandao ya kijamii, vijana hao wa kiume na kike, wenye umri wa miaka 20 wametoa onyo kwa wanasiasa kuwa hali haitakuwa shwari nchini siku zijazo.
Rais Ruto alipata ushindi kupitia uungwaji mkono wa vijana na wanawake katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022, maandamano yao yanaashiria kuwa wamekasirika.
Wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi huo, Rais Ruto aliahidi kuyapa masilahi ya vijana kipaumbele kiasi cha kubuni wizara mahsusi ya vijana.
Hata hivyo, miezi mitatu kabla ya Dkt Ruto kuadhimisha miaka miwili afisini, anakabiliwa na upinzani kutoka kwa tapo hilo la wapiga kura ambalo sasa linahisi walihadaiwa.
Kundi hilo maarufu kama Gen Z, ambalo linatarajiwa kuwa sehemu kubwa ya wapiga kura 2027, sasa limeonyesha kujihusisha zaidi na siasa nchini tofauti na miaka ya nyuma.
Tofauti na maandamano ya siku zilizopita yaliyopangwa na wanasiasa, maandamano ya sasa yalipangwa kupitia mitandao ya kijamii na bila kuhusisha wanasiasa.
Katika miaka ya nyuma, watu wenye umri mdogo walipoteza imani na uongozi wa nchi kiasi cha kujitenga na masuala ya kisiasa.
Kulingana na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Javas Bigambo, kutoridhishwa kwa vijana kunapaswa kuwa onyo kwa tabaka la wanasiasa, haswa walioko katika serikali ya Ruta ambaye ameahidi kuendelea kuongesha ushuru.
Bw Bigambo anasema vijana hao wanaelewana na kushirikiana vizuri kuliko mtindo wa zamani wa ushirikishi wa kisiasa.
Hii ina manaa kuwa huenda nchi inashuhudia mabadiliko mapya katika suala zima la uanaharakati wa kisiasa.
“Serikali haifai kupuuzilia mbali mwamko wa sasa wa kisiasa miongoni mwa vijana ambao utaichangia kupoteza uungwaji mkono kutoka kwa tabaka hili muhimu la wapiga kura,” akaeleza.
Bw Bigambo anasema kuwa serikali itaendelea kukumbwa na upinzani mkubwa ikizingatiwa kuwa Rais Ruto ameshikilia kuwa analenga kuhakikisha kuwa ukusanyaji ushuru umefikia asilimia 22 ya utajiri wa nchi.