Habari za Kitaifa

Manusura pekee wa ajali iliyoua saba Ngata Bridge atambuliwa kuwa afisa wa polisi

April 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MERCY KOSKEI NA VITALIS KIMUTAI

MANUSURA pekee kutoka ajali iliyoua watu 7 jana katika eneo la Ngata, Kaunti ya Nakuru, anapokea matibabu katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Nakuru, baada ya kupata majeraha mabaya.

Konstebo wa Polisi Louis Aoko Ogony, 34, anayehudumu katika Kituo cha Polisi cha Central, jijini Nakuru, alikuwa miongoni mwa abiria saba waliokuwa wakisafiria matatu hiyo ya kibinafsi.

Kamanda wa Polisi katika Kaunti hiyo, Bw Samuel Ndanyi, alithibitisha kuwa polisi huyo alikuwa akielekea Kisii pamoja na watoto wake wawili na dadake.

Aliwapoteza jamaa watatu kwenye ajali hiyo iliyofanyika mwendo wa saa 11.40 alfajiri, ambapo watu saba walifariki. Ajali hiyo ilifanyika katika eneo hatari la Ngata, kwenye barabara kuu ya Nakuru-Eldoret.

Katika Kaunti ya Kericho, watu sita walifariki Jumatatu jioni kwenye ajali ya barabarani katika eneo la Duka Moja.

Ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Toyota Probox na lori, ambapo ziligongana ana kwa ana.

Kulingana na ripoti ya polisi, ajali hiyo ilifanyika mwendo wa saa moja unusu jioni, ambapo watu watano wakifariki papo hapo.

Mkuu wa polisi katika eneo la Bonde la Ufa, Bw Tom Odero, aliwarai madereva kuwa waangalifu barabarani, hasa msimu huu wa mvua.

Manusura huyo alivunjika miguu yake.

Waliofariki walitambuliwa kama Mary Achieng, 15, Godfrey Omwocha Musioma, 34, Jorum Atandi Musioma, 21, Bundi Nyaribo Isaac, 34 na watoto wawili—mmoja wa miaka miaka sita na mwingine wa mwaka mmoja na nusu.

Miili ya marehemu ilipelekwa katika mochari ya Nakuru Anex Hospital ili kuhifadhiwa, huku ikingoja kufanyiwa upasuaji.