• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 12:16 PM
Mapango ya hongo yaangaziwa katika ripoti ya EACC, Nyamira ikiwika

Mapango ya hongo yaangaziwa katika ripoti ya EACC, Nyamira ikiwika

NA BENSON MATHEKA

IKIWA unataka huduma ya aina yoyote katika serikali ya kitaifa na kaunti hasa Nyamira, Baringo, Siaya, Bungoma, Turkana, Pokot Magharibi, Samburu, Nandi, Kakamega na Kisumu jiandae kutoa hongo.

Huu ni ufichuzi wa ripoti ya hivi punde ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuhusu kiwango na athari za ufisadi nchini. Ripoti inasema kwamba, kaunti hizi kumi zinaongoza kwa rushwa huku watu wote wanaotaka huduma wakilazimika kutoa hongo.

Wanaotafuta huduma katika kaunti ya Busia wanaweza kuitishwa hongo mara mbili zaidi wakifuatiwa na wanaofanya hivyo kaunti za Nairobi (mara 1.12 ), Nakuru (mara 1.11) na Machakos ( mara 1.09).

Na iwapo unatarajia kupata maji na chakula cha msaada kutoka kwa serikali kuu au ya kaunti wakati wa janga kama kiangazi, mafuriko au moto, hautaweza iwapo hautatoa hongo.

Tume inasema katika ripoti yake kwamba, ufisadi umekolea katika kaunti hivi kwamba, kila anayetaka huduma ya aina yoyote ikiwemo matibabu ni lazima atoe pesa kuzipata.

Ripoti inasema kwamba, asilimia ya 38.8 Wakenya huwa wanalazimika kutoa hongo kwa kuwa ndio njia ya pekee kupata huduma wanazotaka kutoka kwa serikali huku asilimia 20 wakisema walilipa hongo kwa kuwa waliitishwa ili wahudumiwe.

Asilimia 19 ya Wakenya hulipa hongo ili wahudumiwe kwa haraka katika ofisi za umma.

Na hata baada ya kutoa hongo, kiwango cha huduma wanazopata wakazi ni duni.

“Wengi wa wanaotafuta huduma, ( asilimia 63.8) hawakuridhishwa na huduma za umma walizopata baada ya kulipa hongo. Ni asilimia 36.2 waliosema kuwa waliridhishwa na huduma baada ya kutoa rushwa,” EACC inasema kuhusu ripoti yake ya mwaka 2023.

Katika ripoti hiyo, tume imefichua kwamba Wakenya huwa wanalipa hongo kila wakati wanapotafuta huduma za usalama kutoka kwa polisi na hata wanapotaka kusaidia mtu aliyekamatwa na polisi kuachiliwa huru.

Katika serikali ya kitaifa, Wakenya wanaweza kulipa hongo kusajiliwa kama walimu na Tume ya Huduma ya Walimu, kupata chakula cha misaada, kupata huduma za afya, kusajili au kuhamisha umiliki wa gari, kutafuta leseni ya kuendesha gari, kutafuta basari kutoka kwa Hazina ya Maeneo Bunge (CDF) na kupata huduma kutoka kwa maafisa wa kilimo.

Hii ni baada ya ufichuzi kuwa idara ya polisi wa trafiki, idara ya afya katika kaunti, polisi, idara ya elimu katika kaunti, Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama (NTSA) na ofisi za maafisa wa utawala wakiwemo makamishna wa kaunti na manaibu wao ni mapango ya ufisadi.

Ofisi za maafisa wa utawala zinasimamia misaada ya serikali ya kitaifa wakati wa majanga kama njaa na mafuriko na hii inaeleza kwa nini ripoti inafichua kuwa Wakenya wanaoteseka na njaa wanalazimishwa kutoa hongo kupata chakula cha misaada.

Kwa upande mwingine, afya na kilimo ni moja ya majukumu yaliyogatuliwa na yanasimamiwa na serikali za kaunti ambazo ripoti inataja kama kitovu cha ufisadi katika utoaji wa huduma za kimsingi.

Ripoti ya EACC vile vile inataja ofisi ya hazina ya vijana, ofisi za wawakikishi wa wadi, tume ya utumishi wa umma, Wizara ya Ulinzi na shule za sekondari za umma kama zilizokolewa na hongo.

“Kila wakati mtu anapotafuta huduma za kusajili biashara, nambari ya usajili ya TSC, maji au chakula cha msaada, tenda, kusajili na kuhamisha umiliki wa gari au kupata cheti za ujenzi, huduma za elimu, leseni ya kuendesha gari, pesa za CDF, huduma za kilimo nyanjani na kuhamisha mwanafunzi kutoka shule moja au nyingine ni lazima atoe hongo,” ripoti ya EACC inasema.

Katika serikali za kaunti, kiasi cha juu cha hongo kiliripotiwa katika kaunti ya Pokot Magharibi ambacho ni Sh56,695)Nairobi (Sh 37,768); Murang’a (Sh 18,378); Kisii (Sh 16,810); na Uasin Gishu (Sh 11,136).

Ili kupata huduma katika NTSA, Wakenya walilazimika kulipa hongo ya wastani ya Sh81,801 na wastani wa Sh49,611 katika idara ya mahakama,.

Kwa ujumla, kiwango cha wastani cha hongo katika kaunti kilipanda hadi Sh11,625 mwaka 2023 kutoka Sh6,865 mwaka wa 2022.

Wanaosaka kazi ndio hulipa kiasi cha juu cha hongo cha wastani wa Sh163,260 huku wanaomba pasipoti wakikohoa wastani wa Sh74,428.

Kuripoti kupotea kwa kitu kwa polisi kunagharimu Wakenya Sh20,300 kwa wastani huku wanaotaka stakabadhi za tenda wakikohoa wastani wa Sh17,000.

  • Tags

You can share this post!

Murang’a yapiga marufuku disko matanga, vileo wakati wa...

Serikali ya Taita Taveta vitani kukomboa Mtito Andei na...

T L