Maraga: Tovuti ya SHA kuzimika na orodha ya hospitali kutoweka ni jaribio la kuficha uhalifu
JAJI Mkuu mstaafu, David Maraga, ameitaka serikali kufanya uchunguzi wa kina kuhusu madai ya jaribio la kulaghai Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) kupitia malipo haramu.
Bw Maraga alisema kwamba ufichuzi wa Wizara ya Afya kuwa ilisitisha malipo ya takriban Sh10 bilioni kwa vituo bandia vya afya ni jambo linalotia wasiwasi kuhusu usalama wa mfumo wa afya nchini.
“Kuna jambo zito na la kutisha linaloendelea katika sekta yetu ya afya. Tovuti ya Mamlaka ya Afya ya Jamii ya Kenya ilizimwa. Pia, tovuti ya sajili za hospitali Kenya (KMFR) ilitoweka. Hili si tu jaribio la kuficha uhalifu mkubwa dhidi ya Wakenya bali pia ni ukiukaji wa haki za kikatiba kwa sababu tovuti hizi ndizo zinahifadhi na kuthibitisha kumbukumbu za serikali kuhusu hospitali na vituo vya afya,” alisema Bw Maraga.
Akihutubia waandishi wa habari jana, Bw Maraga alisema matatizo yanayoripotiwa kwenye mfumo wa afya yanajiri huku mamilioni ya fedha yakilipwa kwa vituo hewa visivyofanya kazi.
Kwa msingi huo, Jaji huyo mstaafu ameitaka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuchunguza si tu vituo vilivyolipwa, bali pia watu wanaosimamia mfumo huo.
“Tunataka EACC kufanya uchunguzi na kuwafikisha wote waliohusika mahakamani, hatua lazima zichukuliwe, na hilo ndilo Wakenya wanataka,” alisisitiza Bw Maraga.
Kwa mujibu wake, hitilafu za mara kwa mara katika SHA zimekuwa zikiathiri mamilioni ya wananchi na kusababisha usumbufu mkubwa katika vituo vya afya.
“Mioyo ya Wakenya imejaa maumivu na kukata tamaa hata kabla ya tovuti hii kuzimwa. Hawa ni kina mama, baba, watoto na ndugu zetu wanaoteseka,” alieleza.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuwa mfumo wa afya, ambao unapaswa kuwa uti wa mgongo wa ustawi wa taifa, unatatizika kwa sababu ya ufisadi na kutowajibika.
“Hatuwezi kuendelea kuvumilia mfumo ambapo fedha za walipa ushuru zinapotea gizani bila yeyote kuwajibishwa. Wizara ya Afya pamoja na mashirika ya kitaaluma ya usimamizi wa afya lazima wawajibishwe.”
Vilevile, serikali imetakiwa kutoa taarifa kamili ya malipo yaliyofanywa na SHA, pamoja na orodha ya vituo vya afya vilivyopokea fedha hizo.
Kwa upande mwingine, Katibu Mkuu wa COTU, Francis Atwoli, ametoa wito kwa SHA kupewa uhuru kamili wa kujiendesha, ili kuweza kushughulikia changamoto zinazoikumba kwa sasa.
Bw.Atwoli alisema COTU imekuwa ikitafuta kikao cha dharura na Waziri wa Afya Aden Duale kujadili changamoto za SHA, lakini juhudi zao hazijazaa matunda.
“Changamoto kuu inayokumba SHA ni kwamba shughuli zake zote zinategemea mfumo wa ICT ambao uko chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Afya Dijitali(DHA) na Wizara ya Afya, badala ya kusimamiwa moja kwa moja na SHA,” alisema Bw Atwoli.