Maraga: Wakati nchi ikiomboleza kifo cha Raila, Ruto alikuwa Ikulu akisaini miswada katili
JAJI Mkuu Mstaafu David Maraga amemshutumu vikali Rais William Ruto kwa kutia saini miswada minane wiki jana, akisema hatua hiyo ilisaliti Katiba na kudhoofisa uhuru wa taifa kwa kutumia sheria katili.
Bw Maraga alisema kuwa ni aibu kuwa Rais alitia saini miswada hiyo dhalimu asubuhi ya Jumatano iliyopita hata baada ya kupokea habari ya mauti ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.
“Wakati ambapo taifa lilikuwa likiomboleza kifo cha Raila Odinga, Rais Ruto naye alikuwa katika ikulu akitia saini si mswada moja tu bali miswada minane ambayo inaendeleza ukatili na udhalimu. Ni aibu kuwa rais anaweza akafanya hivi,” akasema Bw Maraga.
Kati ya miswada iliyotiwa saini na kufanyia sheria za awali marekebisho ni Sheria ya Ubinafsishaji, Utunzaji na Usimamizi wa Wanyamapori, Sheria ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi na Matumizi mabaya ya mitandao.
“Serikali itaamua kufanyia kazi watu wake lini? Mara si moja, afisi ya Rais na Bunge la Kitaifa zimepanga njama, zikashirikiana kusaliti nchi yetu na raia wake,” akasema.
Hasa alitaja Sheria ya Ubinafsishaji na Matumizi mabaya ya Mitandao ambayo alisema inavuruga uhuru wa nchi na mali yake.
“Taifa liko wapi kama halina uhuru na mali yake inafyonzwa?” akauliza.
Alisema sheria ya ubinafsishaji ni hatari na inaweka udhibiti wa mashirika ya umma kutoka kwa raia na Bunge hadi kwa afisi ya Rais.
“Sheria hiyo inaweka mchakato wa ubinafsishaji kwenye afisi ya Rais kupitia waziri wa fedha na Mamlaka ya Ubinafsishaji. Waziri wa Fedha sasa ana mamlaka ya kuanzisha mpango wa ubinafsishaji ambao unaweka mashirika mengi ya umma kuwa rahisi kuuzwa,” akasema.
Alitaja vifungu vya 22 na 23 ambavyo vinalazimisha Bunge la Kitaifa kuidhinisha mpango wa ubinafsishaji ndani ya siku 60 na iwapo litakosa kufanya hivyo basi mchakato huo unaendelea ndani ya siku 30 bila kuidhinishwa na bunge.
“Inaudhi zaidi kuwa mpango wa ubinafsishaji uliopitishwa ni halali kwa muda wa miaka minane. Miaka minane shirika liko mikononi mwa afisi ya rais bila kuingiliwa?” akahoji Bw Maraga.
Kuhusu sheria ya kudhibiti mitandao, Bw Maraga alisema lengo ni kudhibiti na kukandamiza wale ambao wanapinga na kukemea maovu ya utawala wa sasa.
“Sasa Kamati ya Kudhibiti Matumizi ya Mitandao na Kupambana na Uhalifu Mitandaoni imepewa mamlaka zaidi ya kufunga tovuti au kuzima apu za simu kwa madai ya kuendeleza shughuli haramu,” akasema Bw Maraga.
Mitandao ya Tiktok, YouTube, Instagram, Facebook na majukwaa mengine ya kijamii ni kati ya yale ambayo jaji huyo mkuu wa zamani alisema inalengwa na sheria hii mpya.
Aliwataka Wakenya wasimame imara na kuzuia majaribio haya ya kudhoofisha ufaafu wa katiba na unyakuzi wa mashirika ya umma.
“Hatutakubali uhuru wa kuzungumza, vyombo vya habari vidhibitiwe na haki, zote zizikwe na Mheshimiwa Raila Odinga,” akasema.
Vilevile alifichua kuwa makundi kadhaa ya haki yanapanga kuelekea kortini kupinga utekelezaji wa sheria hizo alizosema ni katili.