Habari za Kitaifa

Marehemu Were kuzikwa Ijumaa Mei 9

Na BENSON MATHEKA May 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MBUNGE wa Kasipul, Charles Ong’ondo Were, ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi Jumatano usiku jijini Nairobi, atazikwa Ijumaa, Mei 9 2025.

Hii ni kulingana na kamati ya mazishi ya Bunge inayoongozwa na Mbunge wa Homa Bay Mjini, Peter Kaluma.

Safari ya mwisho ya mbunge huyo aliyeuawa itaanza kwa ibada ya misa ya wafu itakayofanyika katika Kanisa Holy Family Basilica Jumatano, Mei 7, kisha mwili wake kusafirishwa hadi kwao kijijini Alhamisi, kabla ya mazishi kufanyika siku itakayofuata.

Gavana wa Homa Bay, Gladys Wanga, ameahidi kusaidia katika maandalizi ya mazishi, ikiwemo kuboresha barabara ya Karabok inayoelekea kwa Were.

Chama cha Orange Democratic Movement (ODM), ambacho kilimpa tiketi ya ubunge kwa vipindi viwili, kitalifunika jeneza la Bw Were kwa rangi za chama hicho wakati wa hafla ya mwisho, kama ishara ya heshima kwa uaminifu wake kwa misingi ya chama.

Ujumbe wa wabunge utafanya ziara  nyumbani kwa marehemu kijijini Jumamosi, Mei 3, ili kuratibu maandalizi na vikundi vya eneo hilo.

Wakati huo huo, upasuaji wa mwili umepangwa kufanyika Jumatatu, ambapo Bunge limetuma Mbunge wa Teso Kaskazini, Oku Kaunya, na Mbunge wa Seme, Dkt James Nyikal, kusimamia shughuli hiyo.

Mipango ya usalama itaongozwa na Bw Kaluma na Mbunge wa Ruaraka, TJ Kajwang’, huku Bunge likitoa wafanyakazi wa ziada kusaidia.

Harambee ya kukusanya pesa kupitia mtandao inafanyika chini ya usimamizi wa Mbunge wa Kabondo Kasipul, Eve Obara, Mwakilishi wa Wanawake Nairobi, Esther Passaris, na Mbunge wa Kigumo, Wangari Mwaniki, kwa michango kutoka kwa wabunge wenzao, huku Gavana Gladys Wanga akikabidhiwa jukumu la kushirikiana na Idara nyingine za serikali.

Nyumba ya marehemu iliyoko Nairobi inasimamiwa na mbunge wa Dagoretti Kaskazini, Beatrice Elachi, Mbunge wa Kisumu Mashariki, Rozah Buyu, na Dkt Obara, kuhakikisha waombolezaji wanaweza kuifikia kutoa heshima zao za mwisho jijini.