Habari za Kitaifa

Masaibu ya Joho yaandama Nassir

June 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA ANTHONY KITIMO

MIAKA miwili baada ya Gavana wa Kaunti ya Mombasa Abdulswamad Nassir kuchukua hatamu za uongozi, masaibu karibu sawa na ya aliyekuwa mtangulizi wake Hassan Joho yameanza kumwandama.

Gavana Nassir ambaye ameonekana kukaza kamba kutetea maslahi ya wakazi amesema atasimama kidete kuhakikisha vijana hawatajiingiza katika mihadarati akiwa uongozini.

Mikakati yake ya hivi karibuni ya kuzuia utafunaji na uuzaji wa muguka inaonekana kutatiza biashara ya mabilioni ya baadhi ya watu serikalini jambo ambalo limeongeza uhasama kati ya Bw Nassir na serikali kuu.

Mzozo huo umeonekana kuingiliwa na serikali ambayo viongozi wa Pwani wanadai kudhalilisha mipango yao ya kunusuru vijana kutokana na utumiaji wa muguka.

Mbunge wa Likoni Mishi Mboko, mwenzake wa Kisauni Rashid Benzimba na yule wa Mvita Masoud Mohammed wameunga mkono Bw Nassir kusisitiza ni lazima muguka kupigwa marufuku kwani ni vijana wengi wameathirika.

“Tunaomba serikali kuu kushirikiana na Kaunti kupunguza matumizi ya zao hilo kwani madhara yake ni makubwa mno,” alisema Bi Mboko.

Kufuatia mzozo huo, Bw Nassir amesema hatatishwa na serikali kuu baada ya maafisa wa kukusanya ushuru kutembelea Kituo chake cha habari cha Radio Rahma kwa madai ya kukiuka ulipaji ushuru.

“Leo watu wamekuja na vitisho. Hii mambo ya kila mmoja anakuja hapa na ukiuliza wadosi wao wanakuambia ya kwamba sio wao wamewatuma. Mimi sitatishwa na KRA ama serikali kuu kwani nina uchungu kuona vijana wakiharibiwa na muguka,” alisema Bw Nassir.

Hapo baadaye, KRA walithibitisha kuwa walifika katika kituo hicho kukusanya habari zaidi baada ya kampuni kususia kulipa ushuru.

Gavana huyo hata hivyo amesema ataendelea kutetea wakazi wa Mombasa licha ya vitisho hivyo.

Masaibu ambayo yanazidi kumuandama Bw Nassir yanaonekana sawa na yale ya Bw Joho ambapo kudinda Kwake kufanya kazi pamoja na serikali ya Jubilee katika muhula wake wa kwanza kabla ya handisheki kulimfanya kuhangaishwa.

Bw Joho na familia yake walihangaishwa na serikali ya Rais wa Nne Uhuru Kenyatta hivyo kuathiri biashara zao.

Lakini baada ya kuungana na serikali kuu, masaibu hayo yaliisha na biashara zao kunoga.

Swali kuu likibaki iwapo Bw Nassir atadumisha msimamo wake ama atalegeza kamba.