Habari za Kitaifa

Mama na mtoto wakwama India baada ya SHA kukosa kulipia bili ilivyoahidi

Na LEON LIDIGU August 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

FIKIRIA ukiambiwa kuwa moyo wa binti yako mwenye umri wa miezi kumi unapiga kwa neema ya muda mfupi.

Fikiria ukifahamu kwamba nafasi pekee ya kuishi ya mtoto wako ni upasuaji mgumu na wa gharama kubwa katika nchi ya kigeni unayoijua tu kupitia runinga.

Ndoto hiyo mbaya iligeuka kuwa ukweli kwa Boniface Nyang’au na mkewe Gladys Nyabonyi Asuku baada ya binti yao, Chloe Agnes Nyang’au, kugunduliwa kuwa na matatizo hatari ya moyo yanayohitaji upasuaji wa haraka nchini India.

Wanandoa hao walifanikiwa kukusanya zaidi ya Sh1.125 milioni kupitia harambee kanisani, michango ya kifamilia, na michango mitandaoni.

Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) iliahidi kugharamia kiasi kilichosalia cha Sh500,000 ahadi takatifu ambayo haikutimizwa.

Baada ya kuchangia NHIF kwa miaka 16 na kulipia bima ya SHA hadi Februari mwaka ujao, familia hii iliitikia ahadi ya serikali kwa imani.

Lakini walipofika Chennai, India, SHA haikutuma fedha wala kutoa mawasiliano yoyote, na kuwaacha wakiwa mateka kwa kuwa na bili kubwa ya hospitali.

Hospitali ilitoa notisi ya kumruhusu mtoto kuondoka Julai 30 2025 lakini SHA haikutuma Sh500,000 ilivyoahidi.

“SHA walinyamaza kimya kabisa,” Boniface alisema kwa hasira.

Mnamo Julai 25, alitembelea ofisi za SHA na kukutana na Jemimah Ntutu ambaye alimweleza kuwa hawafadhili tena matibabu nje ya nchi hata kwa waliokwisha safiri.

Kuanzia Julai 30, hospitali ilianza kutoza faini ya Sh13,000 kwa kila siku ambayo mama na mtoto walibaki hospitalini bila kulipiwa.

Kufikia Agosti 4, kiasi hicho kilifikia Sh65,000. Boniface alilazimika kutumia logbook ya rafiki kupata mkopo na marafiki wengine wakachangia kiasi cha Sh565,000 ili mkewe na mtoto wawaruhusiwe kuondoka hospitalini.

Taifa Leo ilipowasiliana na Dkt Tracey John wa SHA kuhusu sakata hiyo, alikiri kufahamu kisa hicho lakini akasema: “Nenda umuulize Mkurugenzi Mkuu wa SHA, Dkt Mercy Mwangangi. Yeye ndiye anaweza kueleza. Mimi sina mamlaka ya kutoa maelezo.”

Majaribio ya kuwasiliana na Dkt Mwangangi hayakufanikiwa. Hakuweza kupatikana kwa simu wala kujibu jumbe alizotumiwa na mwanahabari.

Katibu wa Afya ya Umma na Viwango vya Kitaaluma, Mary Muthoni, aliahidi kufuatilia kisa hicho.

“Nahitaji kuangalia stakabadhi. Hili ni suala nyeti, na tunahitaji taarifa sahihi kwa sababu kuna Wakenya wengi India kwa sasa,” alisema.

Tafsiri: BENSON MATHEKA