Habari za Kitaifa

Masaibu ya wanafunzi Helb ikichelewa vyuo vikuu vikifunguliwa

Na MERCY SIMIYU August 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Wasiwasi umetanda kwa maelfu ya wanafunzi wapya wa vyuo vikuu huku baadhi ya taasisi zikitarajia kufunguliwa Jumatatu ijayo, na wanafunzi wapya 194,372 wakikabiliwa na hali ngumu ya kuanza masomo.

Baadhi wana hofu ya kuripoti chuoni bila hata senti ya matumizi, huku wengine wakifikiria kutofika kabisa siku ya ufunguzi.

Vyuo vya Chuo Kikuu cha Nairobi, Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT), Chuo Kikuu cha Kenyatta, Chuo Kikuu cha Maseno, Multimedia, na Chuo Kikuu cha Kibabii vinatarajiwa kufunguliwa kati ya Agosti 18 hadi 25.

Hata hivyo, zikiwa zimesalia siku chache tu, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELB) na Hazina  ya Vyuo Vikuu bado hazijathibitisha tarehe halisi ya kutoa fedha za ruzuku na za matumizi  jambo linaloongeza wasiwasi kuhusu ikiwa wanafunzi wapya wataanza safari yao ya kitaaluma bila msaada wa kifedha wanaoutegemea sana.

Lakini Mkurugenzi Mkuu wa HELB Geoffrey Monari alisisitiza kuwa mchakato wa utoaji fedha unaendelea kama ilivyopangwa.

“Tuko katika njia sahihi. Pesa zitakuwa tayari watakaporipoti,” alisema.

Licha ya hayo, baadhi ya wanafunzi waliohojiwa wanasema wako katika hali ya sintofahamu  hawawezi kupanga usafiri au mahitaji ya msingi.

Kwa Elvis Odhiambo, kupata nafasi ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Garissa imegeuka kuwa chanzo cha majonzi. Kijana huyo wa miaka 24 kutoka Kaunti ya Homa Bay alipata alama ya B– katika KCSE ya 2024, na hatimaye kupata nafasi ya kusomea Shahada ya Elimu ya Sayansi baada ya kujaribu mtihani huo mara tatu.

“Siwezi kujiunga kwa sababu hakuna pesa. Niliomba HELB lakini sijapata kitu. Baba yangu amenambia nitafute kazi ya jua kali kwa sababu hatuwezi lipa Sh119,000 kwa mwaka, na hata nauli ni ghali mno. Nimejitahidi sana kufika hapa. Nilikuwa na matumaini kuwa mkopo ungekuja mapema kusaidia angalau nauli na mahitaji, lakini hakuna chochote,” alisema.

Katika mfumo mpya wa ufadhili, wanafunzi wamegawanywa katika makundi matano ya mahitaji ya kifedha, yanayobainisha asilimia ya ufadhili wa serikali, mkopo, na mchango wa familia.

“Nilifurahi sana nilipopokea barua ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Kaimosi Friends kusomea Shahada ya Elimu. Hii ilikuwa ndoto yangu – nafasi ya kujenga maisha, kuinua familia, na kutimiza malengo. Lakini sasa ndoto hiyo imejaa hofu. Karo ni zaidi ya Sh100,000 na siku zimekaribia, lakini fedha ambazo nilitegemea bado hazijatolewa. Sina uhakika kama nitaweza kujiandaa au hata kuripoti. Shinikizo ni kubwa mno. Nikiwaza jinsi familia yangu imejitolea, natetemeka kuona ndoto hii ikitoweka kwa sababu ya kuchelewa kwa fedha,” alisema Lidya Cherop.

Velton Mboga, aliyepata nafasi katika Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki naye anasema hali ni ngumu:

“Karo ni Sh55,000 kwa muhula, mzigo mkubwa kwa wazazi. Baba yangu ni mwalimu mstaafu. Tumeomba HELB lakini hatujui kama tutapata, au kiasi gani. Inatamausha kutojua kama fedha zitakuja kwa wakati,” alisema.

Katika mitandao ya kijamii, Bw Monari alitetea mfumo mpya wa ufadhili, akiomba wadau wote kuuunga mkono, na kuonya kuwa kurejea kwa mfumo wa zamani ni hatari kwa elimu ya juu.