Habari za Kitaifa

Maseneta wachemkia Safaricom kwa kutoa data za wateja katika shutuma za hivi punde

Na COLLINS OMULO November 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KAMPUNI ya mawasiliano ya Safaricom imejipata matatani kuhusiana na madai kuwa imekuwa ikivunja kanuni ya kuweka siri data za wateja wake.

Maseneta wameisuta kampuni hiyo kwa kusaidia maafisa wa usalama kuwaandamana na kuwateka nyara raia kwa kuwapa data za simu za watu hao.

Haya yanajiri wakati ambapo visa vya watu kutekwa nyara na watu wanaodaiwa kuwa maafisa wa usalama vimeongezeka nchini.

Akiibua shutuma dhidi ya Safaricom katika Seneti, Seneta wa Migori Eddy Oketch aliitaka Safaricom kueleza iwapo imeingia katika mkataba na serikali kwamba iwe ikiipa data.

Aidha, aliitaka kampuni hiyo ya mawasiliano ya simu ya mkono kueleza ikiwa wateja wake wamekubali uwepo wa makubaliano kama hayo.

Seneta Oketch pia anaitaka Kamati ya Seneti kuhusu Habari, Mawasiliano na Teknolojia kubaini ikiwa sheria inairuhusu Safaricom kukusanya na kuhifadhi data za wateja, kama vile mahala walipo na kuafuatiliwa simu za wateja hao.

Pia seneta huyo anataka kuelezwa ikiwa kampuni zingine za mawasiliano zimepewa kibali kama hicho au la.

Bw Oketch anaitaka kamati hiyo kuchunguza usalama wa mtindo wa sasa ambapo kadi za laini za Safaricom (SIM card) zinasimamiwa na kampuni ya kimataifa kwa jina Neural Technologies.

Isitoshe, anataka kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Trans Nzoia Allan Chesang’ ipewe nakala ya makubaliano kati ya Safaricom na kampuni hiyo.

Bw Oketch, anayehudumu muhula wake wa kwanza, alilalamika kuwa awali Wakenya wameibua hofu kuhusiana na madai kuwa Safaricom inakiuka sheria na kanuni kuhusu usiri wa data.

“Tunataka kamati hiyo ieleze hali hii ambapo serikali na asasi zake hupata data kutoka kwa safaricom kwa urahisi inapowaandama washukiwa lakini data hizo huwa hazitolewi ili kusaidia kupatikana kwa simu zilizopotea,” akasema Bw Oketch.

“Pia kamati ya Bw Chesang’ itoe maelezo kuhusu mikakati ambayo Safaricom imeweka kulinda data inayotolewa kwa watu au asasi zingine, aidha kutokana na kibali cha mahakama au bila kibali hicho.

Pia nataka Seneti ielezwe ikiwa ni kweli kwamba malalamishi mengi kuhusu ukiukaji wa data za wateja huelekezwa kwa Safaricom ikilinganishwa na kampuni zingine za kutoa huduma za mawasiliano kwa njia ya simu za mkononi,” akaongeza.

Seneta wa Busia Okiya Omtatah alisema sharti kampuni ya Safaricom ikemewe na kuagizwa ifike mbele ya Seneti ili ielezee shughuli zake zinazokiuka sheria za data.

Bw Omtatah pia aliitaka serikali kuchukulia kwa uzito suala la ulinzi wa data za watu binafsi kwa uzito mkubwa.

“Suala la data ni lenye uzito mkubwa kwani huweza kuchangia vifo vya watu. Data zetu hazifai kusimamia kwa namna ambayo inahatarisha maisha yetu. Safaricom ilishutumiwa kwa kusaidia maafisa wa usalama katika kuwateka nyara raia. Hata hivyo, hadi sasa haijajitetea dhidi ya madai hayo,” akasema Bw Omtatah.