Maseneta waibua hofu kuhusu uhaba wa damu nchini
MASENETA wameanzisha uchunguzi kuhusu uhaba wa damu unaoendelea nchini, hali inayosababisha mateso makubwa kwa wagonjwa wanaohitaji huduma ya kuongezewa damu.
Maseneta hao sasa wameelekeza lawama zao kwa Huduma ya Kitaifa ya Uongezaji Damu (KNBTS) wakitaka maelezo ya kina kuhusu hali ya sasa ya huduma hiyo na upatikanaji wa damu.
Kenya huhitaji painti 500,000 hadi 1 milioni za damu kila mwaka, lakini hukusanya kati ya 150,000 na 200,000 pekee. Hali hii husababisha wagonjwa mahututi kutegemea jamaa na wahisani kwa michango ya damu kuokoa maisha.
Kamati ya Afya ya Seneti, inayoongozwa na Seneta wa Uasin Gishu Jackson Mandago, imepewa jukumu la kuchunguza sababu kuu za uhaba huo sugu wa damu na mikakati inayochukuliwa na Wizara ya Afya pamoja na KNBTS kuhakikisha upatikanaji endelevu wa damu.
Hatua hiyo imechochewa na tahadhari iliyotolewa na Seneta wa Machakos, Agnes Kavindu Muthama, kuhusu uhaba mkubwa wa damu nchini.
“Tunahitaji kufahamishwa mikakati ya kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kutoa damu, na kuvunja imani potofu zinazoathiri hatua hiyo ya hisani,” alisema.
Wizara ya Afya imesema zaidi ya Sh2.7 bilioni zinahitajika kuzuia huduma hiyo kufifia kabisa. Hali hiyo imesababishwa na kusitishwa kwa ufadhili kutoka Amerika, uliokuwa ukisaidia miradi muhimu ya Benki ya Dunia ikiwemo ukusanyaji wa damu, upimaji wa magonjwa ya kuambukiza, uchakataji na uendeshaji wa mfumo wa kidijitali wa damu.
Kenya ilipata pigo tangu mwaka wa 2020, Amerika ilipositisha msaada wa Sh2 bilioni kwa huduma za damu. Hali hiyo imezidisha mzozo kwa kukosa ufadhili mwezi uliopita.Seneta Mteule Beatrice Ogola alisisitiza haja ya kuwa na vituo vya kutunza damu kote nchini na kuhakikisha damu inapatikana kwa haraka hasa wakati wa dharura.
“Wagonjwa wengi, si wa ajali pekee, wanategemea damu kuendelea kuishi. Tumeshuhudia vifo vingi kwa sababu damu haipatikani kwa wakati unaofaa,” alisema.
Pamoja na waathiriwa wa ajali, wanawake wajawazito, wagonjwa wa saratani huhitaji damu mara kwa mara.
KNBTS ina vituo sita vikuu vya damu (Nairobi, Embu, Nakuru, Eldoret, Kisumu na Mombasa) na vituo vya kaunti 14 kama vile Machakos, Kisii, Voi, Meru, Thika na vingine.Kabla ya janga la Covid-19, serikali ilikuwa ikikusanya painti 450 za damu kila siku.
Idadi hiyo sasa imeshuka hadi kufikia 120–140 kwa siku.Uhaba huu umeongezeka kutokana na ongezeko la watu, ajali nyingi za barabarani na magonjwa yanayohitaji damu mara kwa mara.
Licha ya mahitaji hayo, changamoto kubwa ni hofu ya watu kuchangia damu kutokana na imani potofu, hofu ya saratani na magonjwa yatokanayo na virusi vya HIV, pamoja na uelewa mdogo kuhusu mchango wa damu katika kuokoa maisha.