Habari za Kitaifa

Maseneta waibua maswali tele kuhusu ukodishaji wa JKIA kwa Adani

Na SAMWEL OWINO September 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MASENETA wameibua maswali manane kuhusu pendekezo la serikali la kukodisha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kwa kampuni ya Adani kutoka India.

Katika mkutano uliochukua saa tano na Waziri wa Uchukuzi, Davis Chirchir Alhamisi, Septemba 12, 2024 Kamati ya Seneti kuhusu Barabara, Uchukuzi na Makazi ilitaka stakabadhi muhimu zikaguliwe kabla ya mkataba wa mwisho kutiwa saini.

Miongoni mwa maswali ambayo maseneta waliibua ni kwa nini serikali isikatishe mpango huo, kwa nini zabuni hiyo haikuwa wazi, wanahisa wa Adani na ripoti kuhusu asili ya Adani.

Kamati hiyo pia inaitaka serikali kueleza wazi iwapo makubaliano hayo tayari yameafikiwa, kwani tayari timu imeshatumwa India na mazungumzo yanaendelea kuhusu kuunda timu ya usimamizi.

Kamati hiyo pia ilihoji jinsi Adani ilipata picha za kipekee za JKIA, pamoja na maeneo ya setilaiti.

Nyaraka zilizowasilishwa kwa kamati hiyo pia zinaonyesha kwamba wasiwasi uliotolewa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (KAA) kuhusu mpango huo katika mkutano wake wa bodi mnamo Juni 2024 ulipuuzwa.

Mukhtasari wa kikao cha bodi hiyo kilichowasilishwa kwa kamati hiyo unaonyesha kuwa katika kikao cha mwezi Juni, bodi ilieleza kuwa mpango huo umevutia watu fulani serikalini hivyo kuwa vigumu kuutekeleza.

“Ilibainika kuwa mradi huo umevutia serikali na ni vigumu kuendelea kuitekeleza.”

Hata kabla ya kuandika ripoti yake ya mwisho, kamati hiyo ilitaka kufutwa kwa mpango huo, ikieleza kuwa ni mpango mbaya kwa nchi.

Seneta wa Busia Okiya Omtatah alisema mchakato mzima ulikuwa wa ulaghai na haukuzingatia sheria jinsi ilivyoainishwa katika Sheria.

“Kinachowasilishwa mbele yetu ni ulaghai, huu unaweza kuwa mchakato wa ufujaji wa pesa zilizoibiwa kutoka kwa Wakenya na sasa zinarejeshwa nchini kwa jina la kujenga uwanja wa ndege,” Bw Omtatah alisema.

Bw Omtatah alisema kabla ya makubaliano hayo kufanywa, sheria inaitaka kampuni hiyo, kulipa ushuru katika nchi husika na kwamba kampuni hiyo inafaa kuonyesha kuwa haina rekodi ya ulaghai.