Masengeli aonya wanasiasa wanaochochea vurugu
SERIKALI imewaonya wanasiasa wanaowachochea na kuwalipa vijana ili kuzua fujo katika mazishi na mikusanyiko mingine ya watu.
Naibu Inspekta Jenerali wa polisi (DIG) Gilbert Masengeli alisema hali hiyo huenda ikasababisha machafuko uchaguzi wa 2027 ukikaribia.
Bw Masengeli, haswa, aliwaonya wanasiasa kutoka Magharibi mwa Kenya ambako visa vya makabiliano makali vimeshuhudiwa katika mazishi.
‘Tunawakujia. Hatutakaa na kutazama mkichochea vijana kuteketeza mashamba ya miwa, kusababisha fujo na kusitisha mazishi,’ alionya.Bw Masengeli alizungumza jana akiwa katika mji wa Kakamega.Aliandamana na Mkurugenzi Mkuu wa DCI Mohammed Ibrahim Amin na Seneta wa Garissa Abdulkadir Mohammed Hajji.
Mbunge wa Lurambi Titus Khamala aliwataka maafisa wa usalama kuwa macho dhidi ya wanasiasa hao kabla ya uchaguzi wa 2027.
“Wacha polisi wafanye kazi yao na kudhibiti mwenendo usiofaa wa kuzua vurugu katika mazishi. Hatutaki wanasiasa wengine wafikirie kuwa wanaweza kuzua vurugu kwa sababu huo ni uhalifu, ” alisema.
“Viongozi waadilifu hawapaswi kuwatumia wahuni kuharibu mazishi. Wacha polisi wawakamate majambazi, hata kama ni mimi kwa sababu huo ni uhalifu,” alisema Bw Khamala.
Katika eneo la Magharibi, visa vya makabiliano kisiasa na machafuko vimeshuhudiwa hasa wakati wa mazishi.Mazishi sasa yamebadilishwa kuwa maeneo ya kujipiga kifua kisiasa,matusi na vurugu, huku wanasiasa wapinzani wakitumia fursa hiyo kuonyesha ubabe wao.
Familia ya Bw Agostino Odongo, chifu wa zamani wa lokesheni ya Wanga Kaskazini huko Matungu ilipata hasara ya mamilioni ya pesa baada ya mazishi ya Februari 8, 2025 kugeuka kuwa ya ghasia baada ya wafuasi wa wanasiasa watatu kukabiliana.
Waandalizi wa hafla hiyo waliipiga familia hiyo faini ya Sh1.5 milioni baada ya uharibifu mkubwa wa mali wakati wafuasi wa Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa walipokabiliana vikali na wale wa aliyekuwa Waziri wa Michezo Rashid Echesa pamoja na wale wa Mbunge wa Matungu Peter Nabulindo.